
Baadhi ya wakulima wa kilimo cha kahawa kijiji cha Utiri Mbinga Mkoani Ruvuma wakiangalia uzalishaji kwenye miche ya kahawa katika moja ya shamba linalomilikiwa na Chama Cha Msingi Ushirika Kimuli Amcos
Baadhi ya wakulima wa kilimo cha kahawa kijiji cha Utiri Mbinga Mkoani Ruvuma wakiangalia uzalishaji kwenye miche ya kahawa katika moja ya shamba linalomilikiwa na Chama Cha Msingi Ushirika Kimuli Amcos
Na Regina Ndumbaro Mbinga.
Wakulima wa zao la kahawa wanaohudumiwa na Chama cha Msingi cha Ushirika Kimuli Amcos, kata ya Utiri, Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wamefanikiwa kuzalisha tani 105,986.95 za kahawa na kupata mapato ya zaidi ya shilingi bilioni 14 kuanzia msimu wa kilimo wa 2021/2022 hadi 2024/2025.
Katibu wa chama hicho, Aron Komba, amesema kuwa katika msimu wa 2021/2022, wakulima walizalisha tani 548,551 zenye thamani ya shilingi bilioni 3.3, huku msimu wa 2022/2023 wakizalisha tani 455,643 na kupata shilingi bilioni 3.06.
Kwa msimu wa 2023/2024, wanachama wa Kimuli Amcos walizalisha kilo 585,288 za kahawa zilizowaingizia shilingi bilioni 2.9, huku msimu wa 2024/2025 wakizalisha kilo 530,253 na kuuza kahawa hiyo kwa shilingi bilioni 4.72 kupitia minada.
Komba ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na jitihada za Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwemo utoaji wa mikopo ya pembejeo zenye thamani ya shilingi bilioni 3.05 kwa wakulima 7,005 wanaojishughulisha na kilimo cha kahawa na mazao mengine ya chakula na biashara.
Katika msimu wa 2022/2023, wakulima walipata mikopo ya pembejeo ya shilingi milioni 957 kwa wanachama 2,137, huku msimu wa 2023/2024 wakipata mikopo ya shilingi milioni 917 kwa wanachama 2,381.
Kwa msimu wa 2024/2025, mikopo ya shilingi bilioni 1.18 ilitolewa kwa wanachama 2,487. Komba alisema mikopo hiyo imewasaidia wakulima kulima kwa tija, kwani awali walikuwa wanapata shida kupata pembejeo zilizokuwa zinauzwa kwa bei kubwa kati ya shilingi 165,000 hadi 170,000 kwa mfuko wa kilo 25.
Kutokana na gharama hizo kubwa, baadhi ya wakulima walikata tamaa na kutoendelea na kilimo, lakini juhudi za Serikali katika kutoa pembejeo za ruzuku zimeleta nafuu kwa wakulima.
Komba ameiomba Serikali kuendelea kutoa pembejeo za ruzuku kwa zao la kahawa ili kupunguza mzigo wa gharama kwa wakulima na kuwawezesha kuzalisha kwa wingi.
Pia, ameshauri Serikali kusaidia ujenzi wa miundombinu ya kukaanga kahawa ili wakulima waweze kuuza kahawa iliyoongezewa thamani badala ya kuiuza ghafi.
Hii itaongeza kipato cha wakulima na kuchangia maendeleo ya sekta ya kahawa nchini.
Makamu Mwenyekiti wa Kimuli Amcos, Yordan Komba, amesema kuwa chama hicho kimepiga hatua kubwa katika kipindi cha miaka minne kwa kuongeza wanachama kutoka 364 mwaka 1993 hadi kufikia wanachama 1,700 mwaka 2024.
Ameiomba Serikali kupitia maafisa ugani kuwapatia wakulima elimu ya mbinu za kilimo cha kisasa ili kuongeza uzalishaji na mavuno.
Mkulima na mwanachama wa Kimuli Amcos, Gisat Komba, amesema kuwa kwa miaka minne iliyopita, uzalishaji wa kahawa umeongezeka kutokana na upatikanaji wa pembejeo za ruzuku zinazotolewa na Serikali.
Hii imehamasisha watu wengi, hasa vijana, kujikita katika kilimo cha kahawa.
Hata hivyo, changamoto kubwa inayowakabili ni soko la uhakika, kwani wanunuzi wana tabia ya kupanga bei bila kuwashirikisha wakulima, jambo linalowaumiza kutokana na gharama kubwa za uzalishaji.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Utiri, Libaba Gervas Libaba, amesema kuwa kata hiyo ni maarufu kwa kilimo cha kahawa na wakulima wake wanajitahidi kulima kwa bidii.
Hata hivyo, changamoto kubwa ni upatikanaji wa pembejeo za ruzuku ameiomba Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Mbinga kukamilisha ujenzi wa barabara ya lami ya Utiri-Mahende ili kuwezesha usafirishaji wa mazao kwa urahisi, kwani barabara hiyo inapita katika maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa kahawa.