NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
BODI ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania -TPDC imeridhishwa na Maendeleo ya mradi ujenzi wa kituo mama cha kushindilia na kujaza gesi asilia-CNG katika eneo la Chuo Kikuu Jijini Dar es Salaam ambacho kinatarajiwa kukamilika ndani ya mwezi huu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 3, 2025 Jijini Dar es Salaam,Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TPDC, Paul Makanza amesema kukamilika kwake kutasaidia kupunguza gharama za ununuzi wa mafuta kutoka nje ya nchi ambayo bei yake ipo juu kuliko gesi ambayo huzalishwa hapa nchini.
Amesema matumizi ya gesi asilia ni mbadala wa mafuta ya petroli na dizeli, hivyo itaiwezesha serikali kuokoa fedha za kigeni zinazoelekezwa katika ununuzi wa mafuta kutoka nje ya nchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji wa TPDC, Derick Moshi amesema kimekamilika kwa zaidi ya asilimia 90 na kinatarajiwa kuanza kutoa huduma hivi karibuni.
Aidha amesema kuwa kabla ya mwezi huu kumalizika, kituo hicho kitazinduliwa rasmi na kuanza kutoa huduma kwa umma.
Mradi huo unaojengwa katika eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam umegharimu takribani Shilingi bilioni 14.5.