Wataalamu wa takwimu wametakiwa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na ufasaha kwa kuwa uwepo wa takwimu sahihi ni muhimu katika kutatua matatizo yanayolikabili taifa.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Nyongo (Mb), leo tarehe 7 Julai, 2025, wakati akifungua kikao kazi cha wataalamu wa Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania kwa mwaka 2024-2025 jijini Dodoma.
Mhe. Nyongo alieleza kuwa maamuzi makubwa ya kisera yanahitaji taarifa sahihi, na takwimu zitakazopatikana kupitia utafiti huo zitasaidia katika kutafuta njia bora ya kupunguza umaskini katika nchi.
Aidha, Mhe. Nyongo alieleza kuwa, kwa mujibu wa takwimu zilizopo sasa, watanzania wengi wanaishi kwa chini ya dola moja ya Kimarekani (1.9). Katika malengo ya Dira ya Taifa ya 2050, Serikali inalenga kuongeza kipato cha mwananchi hadi kufikia Tsh. 4,000 hadi 8,000.
Alisema kuwa hayo ndio matamanio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kwamba jukumu la kuandaa mipango itakayowezesha kipato cha Mtanzania kufikia matarajio hayo wamepewa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji.
Aliongeza kuwa utafiti huu ni muhimu kwani utatoa picha halisi ya hali ya kipato cha kila Mtanzania na kusaidia Serikali kupanga mikakati bora itakayoboresha ustawi wa wananchi. Aidha, aliipongeza Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa mchango wake katika uchambuzi wa takwimu muhimu zinazosaidia maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Mhe. Anne Makinda, alieleza kuwa jumla ya wadadisi 1,000 wamepatiwa mafunzo kwa ajili ya kufanya utafiti huo.
Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Bi. Albina Chuwa, alifafanua kuwa sensa hiyo itasaidia kupima kiwango cha umaskini wa kipato na kutoa mwanga juu ya maeneo yanayohitaji kuboreshwa katika sekta mbalimbali.
Dkt. Chuwa alibainisha kuwa utafiti huu utaenda kufanyika katika mikoa yote ya mijini na vijijini, na aliwahimiza kaya zitakazochaguliwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wadadisi ili Serikali iweze kupata takwimu zitakazotumika katika juhudi za kupunguza umaskini.