Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Nyakimura Muhoji (aliyesimama katikati) akifungua kikao cha kazi cha kupitia Miongozo ya Masuala ya Nidhamu na Ajira inayoandaliwa na Tume, wengine ni Bw. Bambumbile Mwakyanjala (kulia) Mkurugenzi wa Miongozo, Uwezeshaji na Utafiti na Bw. Robert Lwanji (kushoto) Afisa Mwandamizi wa Tume.
Bw. Evarist M. Mashiba, Afisa Sheria Mkuu akiwasilisha mada kuhusu Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298 (marejeo ya mwaka 2019) kwa Wakuu wa Idara, Sehemu, Vitengo na baadhi ya watumishi wa Tume (hawapo pichani) wakati wa kikao cha kazi cha kupitia Miongozo ya Masuala ya Nidhamu na Ajira inayoandaliwa na Tume, kikao cha kazi kinafanyika mjini Morogoro.
Baadhi ya washiriki Bibi Celina Maongezi, (kulia) Katibu Msaidizi, Bw. John Mbisso (kushoto) Naibu Katibu na Maafisa wa Tume wakisikiliza uwasilishwaji wa mada kuhusu Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298 (marejeo yam waka 2019) wakati wa kikao cha kazi kinachofanyika mjini Morogoro.
Mkurugenzi wa Miongozo, Uwezeshaji na Utafiti wa Tume, Bw. Bambumbile Mwakyanjala (kulia) akifafanua jambo kwa washiriki (hawapo pichani) wakati wa Kikao cha kazi cha kuhuisha Miongozo ya Masuala ya Nidhamu na Ajira inayoandaliwa na Tume ya Utumishi wa Umma kinachoendelea kufanyika mjini Morogoro.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Nyakimura Muhoji (kulia) katika picha ya Pamoja na Bibi Rose Elipenda, Naibu Katibu, Bibi Celina Maongezi (wa tatu kutoka kulia) Katibu Msaidizi, Bw. Enos Ntusso, Katibu Msaidizi na Bw. Richard Cheyo (kushoto) Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, wakati wa kikao cha kazi cha kuhuisha Miongozo ya masuala ya Nidhamu na Ajira inayoandaliwa na Tume, kikao kinachofanyika mjini Morogoro.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Nyakimura Muhoji (wan ne kutoka kulia) akiwa katika picha ya Pamoja na Wakuu wa Idara, Sehemu, Vitengo na baadhi ya watumishi wa Tume baada ya ufunguzi wa kikao cha kazi cha kupitia Miongozo ya Masuala ya Nidhamu na Ajira inayoandaliwa na Tume, kikao kinafanyika mjini Morogoro. (Picha na PSC).
**********
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Nyakimura Muhoji amesema uhuishaji wa Miongozo ya Nidhamu na Ajira inayoandaliwa na Tume ya Utumishi wa Umma itawasaidia Waajiri, Mamlaka za Ajira na Mamlaka za Nidhamu kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayotolewa.
Bwana Muhoji amesema haya jana wakati akifungua kikao cha kazi cha Wakuu wa Idara, Sehemu, Vitengo wa Tume na baadhi ya watumishi wa umma kwa lengo la kupitia Miongozo ya Masuala ya Nidhamu na Ajira inayoandaliwa na Tume ya Utumishi wa Umma, kikao kinachofanyika Mkoani Morogoro.
"Ninafahamu kuwa mmekuwa mkitekeleza majukumu yenu vizuri licha ya changamoto mbalimbali zilizotokana na Miongozo iliyotolewa na Tume ya Utumishi wa Umma kupitwa na wakati. Ni imani yangu kupitia kikao hiki mtatekeleza lengo la kuwa hapa la kuiwezesha Tume ya Utumishi wa Umma kuhuisha Miongozo ya Ajira na Nidhamu katika Utumishi wa Umma ambayo itawasaidia Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu katika Kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayotolewa'' alisema.
Bwana Muhoji alitoa wito kwa washiriki wote kutoka Tume na baadhi ya Ofisi za Serikali kutumia fursa ya kikao hiki cha kazi kujadili kwa kina kuhusu Miongozo inayoandaliwa na Tume ili kuiwezesha Tume kukamilisha kazi ya Uhuishaji wa Miongozo kwani michango yao pamoja na uzoefu walio nao kutoka katika vituo vyao vya kazi utasaidia sana katika kubadilishana uzoefu baina ya Tume na hatimaye kuhuisha Miongozo hii ipasavyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miongozo, Uwezeshaji na Utafiti wa Tume, Bwana Bambumbile Mwakyanjala alisema kuwa lengo la Kikao hiki cha Kazi ni kupitia na kujadili Miongozo ya Ajira na Nidhamu ili kuweza kupata maoni na mtazamo wa washiriki kuhusu masuala ya msingi yanayopaswa kuzingatiwa wakati wa kukamilisha kazi ya kuandaa Miongozo husika.
"Kupitia Kikao Kazi hiki nina imani kitawasaidia Watumishi wa Tume kushiriki katika mchakato wa kuhuisha Miongozo inayoandaliwa na Tume na kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu miongozo hii. Vile vile, katika Kikao Kazi hiki kutakuwa na Rufaa zitakazorejewa ili kuweza kupata uwelewa wa pamoja na yale yatakayokubaliwa na washiriki yataingizwa katika Muongozo wa Masuala ya Nidhamu. Aidha, Mada mbalimbali zinazotumika katika Uwezeshaji wa Wadau wa Tume zitawasilishwa na kujadiliwa" alisema Bwana Mwakyanjala.
Tume ya Utumishi wa Umma inatekeleza jukumu hili la uandaaji wa Miongozo hii chini ya Kifungu cha 10(1) (C) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298 (Marejeo ya mwaka 2019).
Imeandaliwa na:
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
TUME YA UTUMISHI WA UMMA
MOROGORO
04 AGOSTI 2021