Thursday, August 5, 2021

Rafiki wa karibu wa kukupa mafanikio ni huyu hapa

 

Kama unataka kusonga mbele na kuwa na mafanikio makubwa zaidi, mshirika wa kwanza ambaye unatakiwa kushirikiana naye bila kumwacha hadi akakupa mafanikio hayo ni muda wako ulionao.
Ufanye muda uwe rafiki yako wa karibu sana ili ukupatie mafanikio. Usipoteze muda wako kwa mambo ya hovyo, fanya vitu vyako kwa umakini na mpangilio mkubwa, kila unapotumia muda wako.

Inawezekana maisha yako umekuwa ukiyaona hayafai hasa kwa kuona hujatimiza karibu kila kitu. Hiyo inaweza ikawa ni sawa, lakini wakati na nafasi ya kubadili mambo hayo na kuwa mazuri unayo tena.

Muda ukiutumia vizuri unaweza kukupa uwezo wa kukamilisha mambo ambayo kwa kawaida yalionekana ni magumu kuweza kuyatimiza. Kipi unachokitaka ambacho kitashindikana kwa sababu ya muda.

Je, unataka kuandika kitabu? andika mistari michache kila siku, muda utafika kitabu chako kitakamilika. Je, unataka kujenga biashara yako? anza na biashara yoyote hata kama ni ndogo sana na ikuze kidogo kidogo, muda ukifika itakuwa kubwa sana.

Chochote unachotaka kukifanikisha kwako inawezekana, hata iwe unataka kuongea lugha mpya? jifunze maneno machache kila siku na wakati utafika utafanya kwa ufasaha na kujikuta mzungumzaji tayari.

Kama nilivyotangulia kusema, karibu kitu chochote unachokitaka, kipo ndani ya uwezo wako na unayo nafasi kubwa ya kukifikia ikiwa utaamua kutenga muda wako kufanya jambo hilo na kulifanikisha.

Rafiki wa karibu yako, rafiki ambaye anaweza kukupa mafanikio makubwa sana  ni muda wako. Unatakiwa ukae chini na kujiuliza maswali ya msingi, je muda wako unautumia vizuri au hovyo hovyo.

Kama unatumia muda wako hovyo, utakuwa kwenye wakati mgumu sana wa kuweza kubadili hali ya maisha yako na hadi kuwa nzuri. Kumbuka hata ukiwa na hali mbaya vipi, lakini ukiweka juhudi na kujipa muda utafanikiwa.

Hakuna ambaye ameachwa mtupu, kama matumizi ya muda wake ni sahihi. Kama ulikuwa hujaanza kutunza muda wako kwa ajili ya mafanikio, anza leo. Fanya mambo ya kukua mafanikio hata kama ni madogo sana, baada ya miaka michache utafanikiwa.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...