Tuesday, August 10, 2021

Polisi Anayedaiwa Kuua Mtoto Aibuka


Askari polisi, Eliud Msangi anayedaiwa kuhusika na mauaji ya mtoto Justine James (14), ameibuka na kudai mtoto huyo alikimbizwa na kupigwa na wananchi wa eneo la Magore B na kumsababishia mauti.

Mtoto huyo alifariki dunia Agosti Mosi mwaka huu wakati akipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Amana na kuzikwa Alhamisi Agosti 6 mwaka huu katika makaburi yaliyopo eneo la Magore B kata ya Mzinga Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam.


Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alitoa maelezo kwa Kamanda wa Ilala afungue jalada ili achunguze malalamiko hayo, kwa ajili ya kutafuta ukweli wa tukio hilo linalolalamikiwa na kama ni kweli hatua za kisheria zichukuliwe.


Akizungumza na Mwananchi jana kwa simu, Msangi alidai siku ya tukio aliwakuta wakazi wa eneo hilo wakimkimbiza mtoto huyo na walipomkamata wakaanza kumpiga na kumsababishia mauti.


Msangi alisema mtoto huyo alikuwa akishirikiana na wenzake kumuibia nyaya za umeme kwenye nyumba yake ambazo zote ziliibiwa.


Alidai mtoto huyo na wenzake, huzichuna waya hizo na kuchukua waya wa shaba na kwenda kuuza.


"Yule mtoto nilikuta anapigwa na wananchi, mimi nilikuwepo lakini sikuhusika kumpiga, hata hivyo mimi siyo msemaji nakushauri mwandishi uende kituo cha polisi Stakishari utapata maelezo yote na shauri nilishalifungua huko," alisema Msangi.


Tukio lilivyokuwa


Ilielezwa kuwa tukio lilipotokea baba mzazi wa marehemu James Msira alisema Agosti Mosi mwaka huu, saa 10 jioni alilipigiwa simu kuwa Justine amepelekwa katika kituo kidogo cha polisi cha Kitunda baada ya kupigwa na jirani yake ambaye ni askari polisi.


Msira alisema kuwa alielekea katika kituo cha polisi hicho na kumkuta Justine akiwa amezidiwa, huku akitupa huku na kule miguu yake


Alisema alimfuata askari polisi mmoja wa kituo hicho na kumweleza kuwa mwanawe amezidiwa, hivyo anatakiwa apelekwe hospitalini.


"Mimi nilipofika katika kituo cha polisi cha Kitunda nilimuona askari polisi ambaye ninamfahamu nilimuuliza kwa nini mtoto wangu mmemuweka ndani wakati hali yake ni mbaya sana na mtuhumiwa aliyefanya hivi ameshakamatwa, sikupata jibu lolote,'alisema Msira.


Aliongeza: "Ninavyofahamu mimi huyu jirani yangu Msangi kituo chake cha kazi kilikuwa kituo cha polisi Keko kwa sasa yupo pale chuo cha polisi Kurasini anasoma kwa ajili ya nyota ya tatu.''


Msira alisema saa tatu usiku walianza safari ya kuelekea katika Hospitali ya Rufaa ya Amana wakati wakiwa njiani mtoto huyo aliga dunia na walipofika hospitalini hapo, madaktari walithibitisha kifo chake na kisha mwili huo kuhifadhiwa.


Shuhuda wa tukio hilo ambaye ni mdogo wa marehemu, Paulo James alisema alikuwa anaelekea stendi saa 9 alasiri wakati anapita karibu na nyumba ya askari polisi huyo, zilisikika kelele za Justine na aliposogea ili ajue kinachomsibu, ndipo alipomuona Msangi akimpiga kwa kutumia gongo. Alimfuata na kumuomba msamaha ili asiendelee kumpiga lakini alikataa.


Alisema alipoona anaendelea kumpiga kwa muda mrefu alipiga kelele, ndipo baadhi ya watu walipojitokeza na hivyo kumfanya Justine apate upenyo wa kukimbia na kuelekea nyumbani.


Alidai kuwa askari polisi huyo alimkumbiza na alipoingia ndani alifunga mlango.


'Watu walijitokeza kumkataza lakini aliendelea kumpiga, kaka yangu alipopata mwanya alikimbilia nyumbani na kuingia ndani lakini huyu askari alimkimbiza alipotaka kuingia ndani mlango niliufunga na ufunguo,"alisema Paulo.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...