Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa
Na Dotto Kwilasa, Dodoma.
MSEMAJI Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amewataka Maafisa Uhusiano na Mawasiliano Serikalini,Wizara, Mashirika na Taasisi kuwa vinara katika kuhakikisha Wananchi wanapata taarifa sahihi ili kuondoa changamoto ya upotoshaji inayoendelea katika jamii na kuleta hofu.
Msigwa ameyasema hayo leo Jijini Dodoma kwenye kikao kazi kati yake Maafisa hao huku akiwataka kuwa wepesi kuisemea Serikali kwenye maeneo yao na kuepusha taarifa za upotoshaji.
Amesema, licha ya tatizo la upotoshaji wa taarifa kuwepo tangu mwanzo,kwa sasa limezidi na kupelekea kukwamisha baadhi ya shughuli za maendeleo hivyo kuwataka Maafisa uhusiano kufanya kazi kwa weledi na wakati ili kuondoa changamoto hiyo.
"Lazima tutimize majukumu yetu kwa kuwa vinara kuhakikisha watu wanapata taarifa sahihi kuihusu Serikali,linapotokea tatizo kama hilo sisi ndiyo tunaopaswa kuwajibika kuisemea Serikali,tusisubiri mambo yaharibike,"amesema.
Mbali na hayo aliwataka pia kuongeza juhudi katika utendaji kazi na kamwe wasiruhusu wananchi kupotoshwa.
"Katika utendaji kazi wenu msikubali kuruhusu kutolewa taarifa za uongo,kumbukeni kuwa vyanzo vya taarifa ni nyinyi naomba hili jambo mlifanyie kazi kwa weledi na nguvu zote,"amesisitiza.
ATAKA KIPAUMBELE VYOMBO VYA HA BARI ZA KIJAMII.
Katika hili, Msemaji huyo wa Serikali ametaka Maafisa Uhusiano na Mawasiliano Serikalini kutopuuza vyombo vya habari vya Kijamii na kusema kuwa haipendezi kuvibagua kwa kuwa navyo vina umuhimu sawa na vyombo vingine.
"Msivipuuze vyombo vya habari za kijamii lazima tushirikiane navyo haipendezi wewe ni Afisa habari wa Taasisi flani halafu unabagua vyombo hivi kana kwamba havifai ,"amesema na kuongeza;
"Lazima mtambue kuwa vyombo hivi vimesajiliwa ili vitumiwe kutoa taarifa mbalimbali kwa jamii,vilevile vyombo hivi hivi mnavyovidharau endapo mtavitumia vitawapa muda wa kutosha kukanusha masuala ya upotoshaji kwa jamii kwa Kuwa ndiyo vipo karibu zaidi na jamii,"
MITANDAO YA KIJAMII
Kuhusu mitandao ya kijamii Msigwa amewataka Maafisa hao kutumia Mitandao vizuri linapokuja suala la akauti za Wizara huku alisisitiza kuwa kuna ulazima wa kuzofanyia kazi Mara kwa mara akaunti hizo na kuleta maana iliyokusudiwa.
"Siamini kwamba siku inaweza kuisha bila kuwa na jambo la kuitaarifu jamii ,wewe usipotumia mtu mwingine ataitumia nafasi hiyo kupotosha,Tovuti za Serikali lazima ziwe hai kufikia lengo la kuhakikisha watanzania wanapata taarifa sahihi,"alisema na kuongeza;
"Tunapotekeleza majukumu yetu kuna njia nyingi za kufikisha taarifa,nitoe wito kwa vyombo vya habari za kijamii kuzingatia masuala ya utoaji wa taarifa sahihi,"amesisitiza.
Msigwa pia aliweka sawa kwenye tatizo la upotoshaji na kusema kwamba sio vyombo vya habari ndivyo vinafanya upotoshaji huo bali ni Mitandao ya kijamii hivyo jamii inapaswa kuwa macho kuelewa usahihi wa habari.