Friday, August 6, 2021

Bilionea Mike Ashely kumuchia mchumba wa binti yake uongozi wa kampuni yake ya mabilioni ya pesa

Mkurugenzi na mwanzilishi wa kampuni ya bidhaa za Michezo Mike Ashley anapaswa kustaafu ili kuongoza biashara zake zingine na kukabidhi hatamu kwa mkwe wake mtarajiwa.

Bodi ya kampuni ya Frasers Group, ambayo pia inamiliki Nyumba ya Fraser, ilisema mazungumzo yalikuwa yakiendelea ya Michael Murray, 31, kumrithi bilionea huyo kuanzia Mei, 1, 2022.

Hatua hiyo inamaanisha Bw. Ashley ataachia madaraka kama mtendaji mkuu lakini atabaki kwenye bodi kama mkurugenzi mtendaji.

Bwana Ashley alianzisha kampuni ya Sports Direct mnamo mwaka 1982 na ana asilimia 64 ya hisa.

Bwana Murray, aliyemchumbia binti ya Bw. Ashley Anna, na kwa sasa ni mkuu anayesimamia maduka ya kisasa ya kampuni hiyo na kubadilisha biashara hiyo.

Chris Wootton, mkuu wa kitengo cha fedha alisema safari ya kumpa Bw. Murray nguvu zaidi imekuwepo kwa muda.

"Michael ni kijana, mwelewa wa kazi yake na anajua mteja anataka nini. Mike ni mzuri sana kwa kuuza soksi", Bw. Wootton aliliambia Gazeti la The Times.

Katika taarifa ya soko la hisa, kundi la kampuni ya Frasers "imependekeza kwamba Bwana Murray atachukua jukumu la mtendaji mkuu, na sasa hivi malipo mazuri yanazingatiwa".

"Bodi inaona inafaa Michael kutuongoza katika safari hii ya mafanikio", kampuni ya Fraser imesema.

Bwana Murray amekuwa akifanya kazi katika kampuni hiyo kwa miaka kadhaa, lakini jukumu lake liliibua maswali baada ya kuibuka Kwa ripoti kuhusu yeye kulipwa mamilioni ya pauni kwasababu ya jukumu la ushauri.

Bwana Ashley, hapo awali alikuwa naibu mwenyekiti mtendaji wa kitengo cha uuzaji rejareja - ambacho kilibadilisha jina lake kutoka Sports Direct International kuwa kundi la kampuni ya Frasers miaka miwili iliyopita - hadi 2016, wakati mtendaji mkuu wa muda mrefu Dave Forsey alipojiuzulu.

Bwana Ashley, mwenye umri wa miaka 56, amekuwa mmoja wa watu mashuhuri tangu alipoanzisha biashara yake.

Kwanza aliingia kwenye tasnia ya mazoezi ya mwili kama mkufunzi kabla ya kufungua duka lake la kwanza la kuuza bidhaa za michezo mtaani huko Maidenhead, Berkshire, mnamo mwaka 1982.

Awali miaka ya 1990, alipanua biashara yake na kufungua maduka mengine aliyoyapa jina Sports Soccer, na kufikia milenia alikuwa na maduka karibu 100.

Baadaye mwaka huo, Bwana Ashley alikua mtu anayejulikana zaidi wakati aliponunua hisa nyingi za klabu ya Newcastle United.

Hata hivyo, utawala wake umekosolewa na mashabiki juu ya mtindo wake wa umiliki na anasemekana kukabiliwa na ukosefu wa uwekezaji.

Hivi sasa anatafuta kuiuza baada ya kuvunjika kwa mkataba wa pauni milioni 300 na kampuni ya Saudi Public Investment Fund.

Mbali na mpira wa miguu, amekuza haraka biashara yake ya rejareja katika miaka ya hivi karibuni, akipiku kampuni kadhaa za Uingereza ikiwa ni pamoja na House of Fraser, Evans Cycles, Jack Wills and Game.

Kampuni hiyo sasa thamani yake ni pauni bilioni 3 na inaendesha biashara zake katika karibu maduka 1,000.

Hata hivyo, kumekuwa na wakati wa kutatanisha.

Mnamo mwaka wa 2016, uchunguzi wa bunge ulimshtumu Ashley kwa kuendesha kampuni ya Sports Direct vibaya kutokana na ripoti ya uchunguzi uliofanywa na Kamati ya Biashara, Ubunifu na Ustadi iliyosema kampuni hiyo "ilikuwa na mazoea mabaya ya kufanya kazi" na kuchukulia "wafanyikazi kama bidhaa badala ya kama wanadamu".

Kampuni hiyo pia imekosolewa sana juu ya matumizi yake ya mikataba ya kibarua cha muda kwa wafanyakazi pale tu inapowahitaji.

Mahakama kuu London ilisikia kwamba mfanyabiashara huyo aliwahi kuandaa mkutano wa usimamizi katika baa moja ambapo alikunywa bia 12 na kutapika kwenye eneo la kuota moto.

Bwana Ashley aliomba msamaha mnamo Machi 2020 baada ya kujitokeza kwa mfululizo wa makosa kwa njia ambayo kundi la kampuni zake zimekabiliana na hatua ya kutotoka nje kwasababu ya ugongwa wa corona.

Mfanyabiashara huyo aliishawishi serikali kuruhusu maduka yake kuwa wazi, akidai " yalikuwa yanatoa huduma muhimu" lakini akabadili uamuzi wake baada ya kukosolewa na wafanyikazi na vyombo vya habari.

Uamuzi wa mfanyabiashara huyo kujiondoa kama mtendaji mkuu ulionekana kushangaza lakini wachambuzi wa biashara za rejareja wamesema wanafikiri bado inaweza kuwa "kama kawaida".

Mchambuzi wa biashara za aina hii Richard Hyman alisema: "Labda kuna hatua hapa ya kumfanya Michael Murray kufahamika zaidi na kuvutia watu kwenye mkakati wake ambao amekuwa akiutumia kuongoza". Nadhani tunahitajika kuwa waangalifu zaidi tusiangalie sana kampuni hii kwa mtazamo wa kikampuni kwasababu haijalishi wana vyeo vipi, hii ni biashara ya Mike Ashley na yeye tu ndiye atakaye kuwa na uamuzi wa mwisho".

Michael Murray ni nani?

Akiwa amehitimu kutoka Chuo Kikuu cha Reading, Bw. Murray alianzisha kampuni yake ya ushauri wa masuala ya majengo na mali mnamo mwaka 2015.

Mmoja wa wateja wake ni kampuni ya Frasers ya Mike Ashley.

Kampuni yake ya ushauri ina jukumu la kutafuta na kujadili mikataba ya duka jipya la Sports Direct na maduka mengine ya rejareja kote ulimwenguni, na pia kutoa ushauri juu ya tovuti zilizopo za kampuni hiyo.

Aliteuliwa "mkuu wa usimamizi wa kampuni ya Frasers mnamo Januari 2019, kazi yake ikiwa kuboresha biashara hiyo kuwa ya kisasa.

Moja ya miradi yake kuu ilikuwa kutengeneza fulana, ambako ni kati ya biashara za Bwana Ashley.

Katika mahojiano na Guardian kufuatia kufunguliwa kwa duka kuu la fulana huko Leicester, Bw. Murray alisema yeye na Ashley walikuwa "wakifanya kazi kama ushirikiano".

 

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...