Wajumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REA) wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Wakili Julius Kalolo, wametembelea Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme Ifakara, mkoani Morogoro na kuwaagiza Wakandarasi kuukamilisha ndani ya muda uliopangwa.
Bodi ilifanya ziara hiyo Agosti 7 mwaka huu wakiwa wameambatana na wataalamu kadhaa kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), akiwemo Mkurugenzi wake Mkuu, Mhandisi Amos Maganga pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya ziara hiyo, Wakili Kalolo alieleza kuwa Bodi imeridhika na Mpango Mkakati uliowasilishwa kwao na Mkandarasi anayejenga Kituo hicho, Kampuni ya AEE kutoka Hispania, ambao umehuishwa kuwezesha ukamilikaji wa Mradi hata kabla ya muda uliopangwa kimkataba.
Akieleza zaidi, alisema Bodi ililazimika kutembelea Mradi huo ili kujionea kwa macho maendeleo yake pamoja na kuzungumza na Wakandarasi baada ya kupata taarifa za kusuasua kwake.
"Kulikuwa na tatizo la ucheleweshaji ambalo mwanzoni lilitokana na tatizo la COVID, hivyo baadhi ya vifaa vilivyotakiwa kuletwa havikuletwa kwa wakati," alifafanua Mwenyekiti huyo wa Bodi.
Aidha, aliongeza kuwa kulikuwa na tatizo la kiutawala "ambapo wataalam muhimu wa Mkandarasi waliopaswa kusimamia utekelezaji wa kila siku wa Mradi hawakuwa wakiishi katika eneo hilo ili kufanya kazi yao ipasavyo."
Hata hivyo, alisema Bodi hiyo ilifanya ziara katika Mradi husika Januari mwaka huu na kutoa maelekezo kuwa udhaifu wote uliopo ufanyiwe kazi na ndiyo lengo la kutembelea eneo hilo tena ili kujiridhisha endapo maelekezo yao yalizingatiwa.
Wakili Kalolo alisema kuwa pamoja na Bodi kuridhishwa na Mpango Mkakati uliohuishwa, bado imebaini upungufu wa wafanyakazi na hivyo imeelekeza idadi yao iongezwe ili wafanye kazi kwa kasi zaidi na viwango zaidi kama ilivyokusudiwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Maganga alibainisha kuwa Bodi na Ujumbe wote wa Serikali ulioshiriki ziara hiyo una imani kuwa endapo Wakandarasi watatekeleza kikamilifu Mpango Mkakati waliouhuisha, hakuna shaka kuwa Mradi utakamilika ndani ya wakati uliopangwa.
Zaidi, aliongeza kuwa, REA imejipanga kufuatilia utekelezaji wa Mradi huo hatua kwa hatua ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na viwango vya juu ili uwanufaishe wananchi waliokusudiwa kama Serikali ilivyodhamiria.
"Bodi imetoa maelekezo, sisi jukumu letu kama REA ni kuhakikisha maelekezo hayo yanatekelezwa kikamilifu," alisema Mhandisi Maganga.
Kwa upande wa Mkandarasi anayejenga Kituo hicho, Kampuni ya AEE, aliwaambia waandishi wa habari kuwa watatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Bodi ili kuhakikisha Mradi unakamilika kwa wakati.
"Tumeahidi kukamilisha kazi hata kabla ya wakati na tutafanya hivyo. Kufikia Novemba mwaka huu tutakuwa tumefikia asilimia 50 ya utekelezaji wa Mradi na ifikapo Aprili, 2022 tutakuwa tumekamilisha Mradi na kuwawezesha wananchi kuwa na umeme wa uhakika zaidi," alisisitiza Mhandisi Francis Kahumbi, Meneja Mradi kutoka kampuni hiyo ya ukandarasi.
Akielezea kuhusu Mradi huo, Meneja Mradi Ifakara (TANESCO), Mhandisi Didas Lyamuya, alisema umegawanyika katika sehemu mbili ambazo ni ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme pamoja na usambazaji umeme katika vijiji 8 na vitongoji 7.
Alieleza kuwa Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme unatekelezwa na Kampuniya AEE kutoka Hispania huku ule wa kusambaza umeme ukitekelezwa na Kampuni ya Burhan kutoka Kenya.
Alisema malengo ya Mradi huo unaofadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (European Union – EU) ni kuwa kwa upande wa Kituo cha Kupoza umeme, kiwe kimekamilika ifikapo Mei, 2021 na usambazaji umeme uwe umekamilika ifikapo Machi, 2022.
"Natoa rai kwa wananchi wawe na moyo kwamba Serikali ya Tanzania, chini ya Uongozi wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wetu Mama Samia, inahakikisha kwamba Mradi huu unatekelezwa kwa kiwango ambacho kimekusudiwa na ndani ya muda uliopangwa."
Mhandisi Lyamuya alisema yeyé pamoja na wasimamizi wenzake wa Mradi watafanya kazi kwa uadilifu na weledi ili kuhakikisha maelekezo ambayo yamekuwa yakitolewa na viongozi wa Wizara ya Nishati na REA yanatekelezwa kikamilifu.