Tuesday, July 13, 2021

Wafanyabiashara wahamishwa Kariakoo, wasamehewa ushuru

Wakati akitaka barabara zote zote zinazoingia Soko Kuu la Kariakoo kubaki wazi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amewashauri wafanyabiashara wa shimoni kuhamia Soko la Kisutu na Machinga Complex na kutolipa ushuru kwa kipindi cha miezi miwili.

Uamuzi huo ameutangaza leo Jumatatu alipotembelea sokoni hapo kukagua maendeleo ya uzimaji moto unaofanywa na Jeshi la Zimamoto na Uoakoaji.

Awali Makalla aliwataka wafanyabiashara kutokuwa na haraka ya kurudi kwenye jengo hadi Serikali itakapojiridhisha na usalama wake kisha kuandaa namna watakavyochukua mali zao.

"Kwa wafanyabiashara wa soko dogo wanaweza kuendelea na shughuli zao kutokana na kutoathiriwa sana na moto uliotokea. Kwa wale wanaoendesha shughuli kwenye hifadhi ya barabara ya kuingia sokoni mnapaswa kuondoka ili ibaki wazi kwa matumizi mengine," amesema Makalla.

Aidha Makalla amesema usalama kwenye soko kubwa bado haujawa sawa hivyo amewashauri wafanyabiashara kuchukua mali zao na kuhamia Soko la Kisutu na Machinga Complex hadi marekebisho yatakapofanyika.

"Kwa Soko la Shimoni ambalo halijaathiriwa kwa kiasi kikubwa, ufanyike utaratibu ili wafanyabiashara wachukue mali zao na kuhamia masoko mengine kutokana na kukosekana kwa umeme," amesema.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...