Tuesday, July 13, 2021

Ripoti ya Marekani yazihusisha China, Ethiopia, Myanmar na ukatili

Washington | Anti China Protest Uiguren Genozid Abstimmung GroßbrittanienSerikali ya Marekani imeendelea kushikilia msimamo wake kuhusu madai kwamba China inahusika na mauaji ya kimbari na ukandamizaji dhidi ya Waislamu wa Uighur na jamii nyingine za watu wachache kwenye jimbo la Xinjiang.

Ripoti ya mwaka ya Wizara ya Mambo ya Nje iliyosomwa siku ya Jumatatu kwenye Bunge la Marekani, imeeleza kuwa Marekani inarudia kusisitiza kwamba serikali ya China imehusika na mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya ubinaadamu kwa jamii ya Uighur, katika jimbo hilo lililoko kaskazini magharibi mwa China.

Ripoti hiyo ya Elie Wiesel inayopinga mauaji ya kimbari na ukatili, imesema uhalifu dhidi ya ubinaadamu unajumuisha kuwafunga, kuwatesa na kuwafunga kizazi kwa lazima ili wasiendelee kuzaliana. Ripoti hiyo imeitaka serikali ya Marekani kuelezea hatua inazochukua kuzuia ukatili unaofanywa ulimwenguni kote na kuhakikisha inaendelea kutetea haki za binaadamu duniani.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Rais Joe Biden amefuata njia ya watangulizi wake katika kuweka vikwazo kwa nchi zinazodaiwa kuhusika na uhalifu dhidi ya ubinaadamu. Marekani inaendelea kuamini kuwa vitendo vya China dhidi ya jamii ya Uighur ni sehemu ya mauaji ya kimbari.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken mara kadhaa amesisitiza kuwa serikali zilizopita za nchi hiyo zimedai kwamba Jamhuri ya Watu ya China inahusika na mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya ubinaadamu kwa watu wa Uighur. China imeendelea kukanusha madai ya kuwazuia watu katika vituo kwenye jimbo la Xinjiang.

Aidha, ripoti hiyo imeonya kuwa nchi za Eritrea, Ethiopia, Myanmar na Sudan Kusini huenda zikakabiliwa na vikwazo zaidi kwa kufanya operesheni ya kuangamiza jamii fulani, kwa kushiriki kwenye mizozo ya mataifa jirani au ndani ya nchi zao wenyewe. Matokeo hayo yalitangazwa awali na serikali iliyopita ya Marekani ya Donald Trump, ikisema Myanmar inahusika katika operesheni ya kuangamiza jamii ya Waislamu wa Rohingya, kwenye jimbo la Rakhine.

Ikulu ya Marekani imesema itaendelea kushirikiana na washirika wake kuishinikiza serikali ya kijeshi ya Myanmar kusitisha aina zote za ukatili, ikiwemo ukandamizaji dhidi ya watu wanaopinga mapinduzi ya mwezi Februari, pamoja na ghasia zinazofanywa dhidi ya jamii ya Rohingya.

Kwa upande wake Ethiopia na Eritrea zinahusishwa na mauaji ya kikabila dhidi ya wapinzani katika jimbo la Tigray. Mwezi Machi Blinken aliliambia bunge la Marekani kwamba vitendo vinavyofanyika Tigray ni sawa na operesheni ya kuiangamiza jamii ya watu wa Tigray.

Sudan Kusini imetajwa katika ripoti hiyo kutokana na kuzorota kwa usalama na kuwepo kwa mauaji ya kikabila, unyanyasaji wa kingono na matumizi ya chakula kama silaha ya vita. Ripoti hiyo inataka wote waliohusika na ukiukaji wa haki za bindaamu Sudan Kusini wafikishwe katika vyombo vya sheria.

Aidha, ripoti hiyo imesema serikali ya Biden itaendelea kuunga mkono juhudi za kuwafikisha katika vyombo vya sheria wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS kutokana na ukatili walioufanya dhidi ya jamii ya watu wachache nchini Iraq na Syria. Pia imerudia nia za Marekani kumtaka Rais wa Syria Bashar al-Assad na serikali yake kuwajibika kutokana na ukandamizaji walioufanya.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...