Monday, July 19, 2021

Tozo za Mitandao ya Simu, Fursa Mpya kwa Wanaume


Mwaka 2014, wakati michuano ya kombe la dunia inafanyika Brazil, ratiba zake zilikuwa zimekaa kushoto sana na muda wa hapa Tanzania. Yaani wakati kule mechi inachezwa saa 12 jioni, huku kwetu ilikuwa ni usiku mnene wa saa sita.


Kwa hiyo, wapenzi wa soka ilikuwa ni lazima aidha wakae macho mpaka muda huo au walale kisha saa 6 usiku waamke kuangalia mechi.


Utaamini kwamba kuna baadhi yetu wanaume tulitumia mpishano huo wa muda kama kisingizio cha kutorudi nyumbani. Mtu anakaa baa mpaka saa 10 alfajiri, akirudi akiulizwa kulikoni, anajibu kilaini tu, nilikuwa naangalia kombe la dunia.


Wakati Covid-19 inaanza, wakati kuna taharuki ya kwamba ukiingia nchini ni lazima kwanza uwekwe karantini siku 14, kuna watu walitumia hiyo kama gia ya kutorudi nyumbani.


Yaani mtu anakaa nje siku 14 kuanzia mwisho wa mwezi anapolipwa mshahara mpaka pesa itakapoisha… kisha akirudi, akiulizwa kulikoni, anajibu kilaini tu, tuliwekwa karantini mke wangu, siku 14. Na hapo sio kwamba alitoka nchi nyingine, alikuwa hapa hapa Tanzania.


Hata wakati yanatokea mabomu Gongolamboto, watu wakawa wanakimbia kwa taharuki huku na kule, kuna wanaume bila kujali uzito wa lile tatizo, na wenyewe wakajiingiza kwenye orodha ya wahanga wa mabomu. Mtu anaishi Msasani mbali na yalikolipuka mabomu anajipoteza nyumbani, kisha baada ya wiki mbili anarudi, akiulizwa ulikuwa wapi, kiulaini kabisa anajibu, nilikimbia mabomu mke wangu. Wanaume tunajua sana kucheza na fursa.


Tunajua kucheza na fursa kiasi kwamba kwa sasa, wakati karibu kila mtu anapiga mayowe na kulalamika kuhusu kutambulishwa kwa tozo ya miamala ya simu ambayo itaongeza makato kwenye kutuma na kutoa… kuna wanaume tayari wameshaitumia hiyo kama fursa kupotea nyumbani au kupata vitu vizuri.


Usishangae ukiambiwa ndani ya siku hizi mbili tatu tayari kuna mdada aliomba pesa kwa kijamaa chake, kivulana chake, akaambiwa; 'baby njoo nyumbani uchukue,'.


Msichana akikumbusha kwa nini? Mbona mitandao ya simu ina huduma ya kutuma na kupokea pesa, si unitumie humu, jamaa anajibu kiulani tu, makato makubwa sana, njoo uchukue… ni mtego huo, ni kunasa kwenye mtego kama kutumia choo ulichokiona ndotoni, wanaume tunajua kutumia fursa.


Kuna wengine, niamini mimi watarudi nyumbani alfajiri, wakirudi wataulizwa ulikuwa wapi, watajibu… nilipeleka pesa tunazodaiwa, na hapo mwenye deni anaishi nje ya mkoa. Mke atauliza, Kwa nini? Unawezaje kusafiri kwenda nje ya mkoa kulipa deni wakati mitandao ya simu ina huduma ya kutuma na kupokea pesa? Jamaa atajibu kiulaini tu, makato makubwa. Wanaume tunajua kucheza na fursa.


Ilimradi kila jambo linapotokea tunataka kuangalia fursa ya kumaliza mambo yetu, mara nyingi yasiyopendwa na familia zetu.


Hili la miamala nalo naiona fursa ndani yake tusubiri pamoja tuone.


Source: Mwananchi

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...