Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan
Rais Samia Suluhu Hassan ameguswa na malalamiko ya wananchi kuhusu tozo za miamala ya simu iliyoanza kutumika hivi karibuni na kuwaagiza mawaziri husika kutafuta suluhisho.
Hayo yamesemwa leo Julai 19,2021 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba kupitia televisheni ya Channel Ten, akisema pia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa na kikao na mawaziri husika ili kutafuta suluhisho.
"Tayari Mheshimiwa Rais ameshaguswa na jambo hili amesikia maoni ya Watanzania wote na amesema tuyafanyie kazi jambo hili," amesema Waziri
Dk Mwigulu ameongeza kuwa suala hilo linafanyiwa kazi na Waziri Mkuu. "Vilevile Waziri Mkuu ameitisha kikao kitakachofanyika kesho (Julai 20) kuendelea kupitia jambo hilo hilo."
Amesema Serikali imesikia kilio cha wananchi na kuna mambo watakayoyafanyia kazi na mengine wataendelea kuwaelimisha wananchi.
"Tumepokea maeneo ambayo yanahitaji kufanyiwa uelewa zaidi kwa maana ya uelimishaji zaidi ili kuwa na uelewa wa pamoja, ikiwa pamoja na viwango vinavyokatwa, yupi anayekatwa, ukataji wakati wa kutoa na mantiki ya jambo hili zima kwa ujumla," amesema.
SOMA ZAIDI HAPA
CHANZO MWANANCHI