Monday, July 12, 2021

RC SENGATI ASEMA LAZIMA KIONGOZI WA CHADEMA ALIYESEMA SHINYANGA IMEELEMEWA NA WAGONJWA WA CORONA ACHUKULIWE HATUA KALI ZA KISHERIA

 

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk, Philemon Sengati, kulia akizungumza na wagonjwa wa Corona alipowatembelea katika Hospitali ya Rufaa mkoani humo, ambapo alikuta hakuna idadi ya wagonjwa wengi kama ilivyoenezwa kwenye mitandao ya kijamii.

Na Marco Maduhu, Shinyanga.
SERIKALI mkoani Shinyanga, imekanusha taarifa ambazo imedai ni za uongo zilizosambazwa na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA (BAVICHA) mkoani Iringa, Vitusi Nkuna kupitia mitandao ya kijamii, kuwa Mkoa wa Shinyanga umelemewa na wagonjwa wa Corona, na ina uhaba wa Mitungi ya Oksijeni.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk. Philemoni Sengati, amekanusha taarifa hizo leo wakati akizungumza na watumishi wa Serikali, na alipo watembelea wagonjwa wa Corona ambao wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga. 

Alisema baada ya kuona tarifa hizo mtandaoni ambazo zimezua taharuki, ndipo akaona ni vyema atembelee pia katika Hospitali ya Rufaa mkoani humo, ili kujionea mwenyewe hali halisi, na kukuta hakuna idadi ya wagonjwa wengi kama ilivyo enezwa kwenye mitandao ya kijamii na Mwenyekiti huyo wa BAVICHA.

"Serikali ya Mkoa wa Shinyanga, tumesikitishwa sana na taarifa hizi ambazo zimeenezwa kwenye mitandao ya kijamii na Mwenyekiti wa BAVICHA mkoani Iringa Vitus Nkuna, kuwa tumeelemewa na wagonjwa wa Corona na hatuna Mitungi ya Oksijeni kitu ambacho ni uongo,"amesema Dk.Sengati.

"Mwenyekiti huyu wa BAVICHA lazima Serikali tumchukulie hatua kali za kisheria kwa kuzusha uongo na kuleta taharuki kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga, hatukatai wagonjwa ni kweli wapo, lakini siyo wengi kama inavyoenezwa na wanaendelea kupata matibabu,"ameongeza.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa, akiwa katika Stendi ya Mabasi ya kwenda wilayani, amewataka wananchi wa Shinyanga kuendelea kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huo wa Corona, kwa kunawa mikono kwa sabuni na majitiririka, kuvaa barakoa, kupaka vitakasa mikono, pamoja na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga DK. Yudas Ndungile, aliwataka wananchi pale wanaposikia dalili za ugonjwa huo, wawahi kwenye huduma za afya, huku akitaja vituo ambavyo vimetengwa kwa ajili ya kutoa huduma hiyo, kuwa ni Hospitali ya Rufaa, Kolandoto, kituo cha afya Kambarage.


Aidha Dk. Ndungile alitaja vituo vingine kuwa ni Kituo cha afya Tinde, Bugarama, Nyamilangano, Hospitali ya Iselamagazi wilayani Shinyanga pamoja na Hospitali ya wilaya ya Kahama, huku akitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni kuchoka, kusikia homa, viungo kuuma, kushindwa kupumua vizuri, na kuharisha.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk, Philemon Sengati, akizungumza katika Hospitali ya Rufaa mkoani Shinyanga na kuwataka wananchi wa Mkoa huo kuendelea kuchukua Tahadhari ya kujikinga na ugonjwa wa Corona.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk. Yudas Ndugile, akielezea dalili za ugonjwa wa Corona wimbi la Tatu, huku akibainisha vituo vilivyotengwa kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wa Corona.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa mkoani Shinyanga Luzila John, akielezea hali ya wagonjwa wa Corona Hospitalini hapo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk. Philemon Sengati, akiendelea kutoa elimu kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ya kujikinga na Corona katika Stendi ya Mabasi.
Elimu ya kujikinga na Corona ikiendelea kutolewa.
Elimu ya kujikinga na Corona ikiendelea kutolewa.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk, Philemon Sengati akiendelea kutoa elimu ya kujinga na Corona katika Stendi ya Mabasi.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk, Philemon Sengati, akinawa mikono ya majitiririka katika Stand ya Mabasi alipowasili kutoa elimu ya kujikinga na Corona.
Awali watumishi wa Serikali mkoani Shinyanga wakitakiwa kuchukua tahadhari ya kujikinga na Corona maofisini mwao.
Awali watumishi wa Serikali mkoani Shinyanga wakitakiwa kuchukua tahadhari ya kujikinga na Corona maofisini mwao.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk. Philemon Sengati, kushotom akiwa na Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa mkoani Shinyanga Dk, Luzila John, alipowasilia kuwajulia hali wagonjwa wa Corona.

Na Marco Maduhu Shinyanga.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...