Makao makuu ya kanisa Katoliki ulimwenguni Vatican, imesema kiongozi wa kanisa hilo Papa Francis yuko katika hali nzuri siku moja baada ya kufanyiwa upasuaji katika eneo la utumbo mkubwa, uliodumu kwa muda wa saa tatu.
Hata hivyo msemaji wa Vatican Matteo Bruni amesema Papa Francis atasalia hospitalini kwa takriban siku saba.
Vatican imetoa maelezo kidogo kuhusu upasuaji huo lakini gazeti moja la Italia liliripoti kwamba madaktari walilazimika kukata karibu nusu ya utumbo baada ya kugundua matatizo ambayo hayakuwekwa wazi.