Tuesday, July 6, 2021

Dk Ndumbaro ataka ubunifu FITI



 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro amewataka watendaji wa Chuo cha Viwanda vya Misitu (FITI) kuwa wabunifu katika uzalishaji wa bidhaa za misitu hatua aliyoeleza kuwa itaboresha utendaji kazi na kutatua changamoto zinazowakabili.

Pia amekitaka chuo hicho kilichopo mjini Moshi Mkoa wa Kilimanjaro kuwa tayari kuhamia Mafinga ili kufikia soko la mazao ya misitu kwa urahisi zaidi kutokana na kupatikana kwa eneo kubwa kuliko ilivyo Moshi.

Ametoa kauli hiyo  alipofanya ziara ya kutembelea chuo hicho na kujionea kinavyofanya kazi pamoja na kusikiliza changamoto zinazokikabili.

Amesema watendaji wana kazi ngumu ya kuhakikisha wanafika palipokusudiwa kwa kuwa wabunifu katika uzalishaji wa bidhaa za misitu ili kuboresha utendaji kazi.

"Kama upo hapa na unaona hauna ubunifu wowote omba kuachishwa kazi na katibu mkuu wa wizara. Tumekuwa na mashine mnazosema zimepitwa na wakati ila zilizalisha tujiulize fedha iko wapi? Tubadilishe malighafi kuwa fedha," amesema Ndumbaro.

Akizungumzia kuhama kwa Chuo hicho, Dk Ndumbaro amesema eneo la Mafinga lina viwanda vingi vya watu binafsi hali itakayorahisishia wanafunzi wa chuo cha FITI kupata maeneo mengi kwa urahisi ya kufanya mazoezi kwa vitendo ikiwa ni pamoja na chuo kupata eneo la hekta 120.

"Wizara tumekuja na mkakati wa kuhamisha taasisi nyingi, TAWA watatoka Morogoro na kuhamia Dar es salam, TFS watatoka Dar es salaam na kuhamia Kanda ya Zziwa na FITI watatoka Moshi na kuhamia Mafinga, hili haliepukiki," amesema.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...