Majambazi nchini Nigeria wamedungua ndege na kuidondosha katika tukio la nadra la kuangushwa kwa ndege ya kijeshi na genge la uhalifu nchini humo.
Rubani alikuwa amekamilisha uvamizi dhidi ya watekaji nyara wakati aliposhambuliwa kwa risasi, limesema jeshi la anga.
Rubani wa ndege hiyo Luteni Abayomi Dairo alifanikiwa kutoka ndani kwa kutumia "mbinu za kujiokoa" ili kuepuka kukamatwa na baadaye akatafuta mahala pa kujihifadhi, kabla ya kujiunga tena na wenzake.
Shambulio hilo lilitokea kwenye mpaka wa kaskazini uliopo baina ya majimbo ya Zamfara na Kaduna.
Magenge yenye silaha –yanayoelezewa na wakazi wa eneo hilo kama ''majambazi''-yamekuwa yakilaumiwa kwa msururu wavitendo vya utekaji nyara katika eneo hili la kaskazini mwa Nigeria.
Wanafunzi na watoto wa shule wamekuwa wakilengwa na utekaji huo-huku zaidi ya 1000 wakiripotiwa kutekwa nyara tangu mwezi wa Disemba. Wengi wao wameokolewa, baada ya kulipa kikombozi, lakini baadhi yao wamekuwa wakiuawa.
Katika siku za hivi karibuni, Rais Muhammadu Buhari aliagizajeshi kufanya liwezekanalo kuwamaliza wahalifu katika majimbo ya Katsina, Zamfara na Kaduna.
Kikosi cha anga cha Nigeri-The Nigerian Air Force kimesema kuwa kimeanza harakati za usiku na mchana dhidi ya majambazi kwa ushirikiano na kikosi cha ardhini. Ilikuwa ni katika maojawapo ya harakati hizo ambapo moja ya ndege zake aina ya jet ilidondoshwa.