Mkuu wa wilaya ya Kahama , Festo Kiswaga akielezea kuhusu maonesho ya biashara ya kimkakati ya wawekezaji, wafanyabiashara na wajasiriamali yatakayofanyika Mjini Kahama kuanzia Julai 30,2021 hadi Agosti 8,2021
Na Patrick Mabula , Kahama.
Serikali wilayani Kahama imeandaa maonesho ya biashara ya kimkakati ya wawekezaji , wafanyabiashara na wajasiriamali wapatao zaidi ya 450 wa ndani na nje ya nchi kwa lengo ya kukuza uchumi na masoko.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 20,2021 ofisini kwake Mkuu wa wilaya ya Kahama , Mhe. Festo Kiswaga amesema maonesho hayo yatafanyika kwa siku kumi kuanzia tarehe Julai 30 hadi Agosti 8,2021 katika Viwanja vya Kahama Mji Zamani (Nyihogo Mjini Kahama) kwa lengo la kutangaza fursa za kiuchumi na uwekezaji zilizopo wilayani Kahama.
Amesema maonesho hayo makubwa ya uwekezaji na biashara yanayoandaliwa na serikali ya wilaya ya Kahama , pamoja na halmashauri zote tatu zilizopo ambazo ni Ushetu , Msalala na Manispaa ya Kahama yanakidhi vigezo vyote vya kibiashara kutokana na fursa mbalimbali za kiuchumi na masoko zilizopo wilayani Kahama.
Kiswaga amesema wilaya ya Kahama yenye watu wanaokadiriwa kuwa zaidi ya milioni moja kwa mujibu wa sensa ya taifa ina vigezo vyote vya uwekezaji katika swala ya kibiashara kutoka na kuwepo kwa fursa nyingi za kiuchumi kwenye madini , kilimo , mifugo na biashara na ipo katika barabara kuu ya rami inayounganisha nchi za maziwa makuu na kiwanja cha ndege.
Amesema maonesho hayo ya kimkakati mbali na kuhusisha washiriki hao zaidi ya 450 pia yanahusisha taasisi zote za umma na serikali pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo na kwa kuzingatia fursa za kiuchumi zinazopatikana katika sekta ya madini, kilimo, ujenzi wa viwanda, elimu, burudani na michezo lengo kufungua masoko kiuchumi.
"Ndugu zangu waandishi wa habari katika maonyesho hayo kutakuwa na mikutano ya kibiashara , mafunzo mbalimbali ya elimu toka taasisi za umma na binafsi na za kifedha zinazohudumia wafanyabiashara na wajasiriamali ili kuwajengea uwezo wa kuwa tija katika shughuli zao", amesema Kiswaga.
Kiswaga amesema wito wake kwa wawekezaji , wafanyabiashara na wajasiriamali na wananachi wote kujitokeza kushiriki ili kuwa na tija kwa maslahi mapana katika kukuza uchumi wao na taifa.
Amesema pia maonesho hayo yatatoa fursa ya watu kuona wanyama pori wakiwemo simba , chui, fisi , mamba na kobe wakubwa kwa lengo la kuhamasisha utalii wa ndani.
Kwa upande wao baadhi ya wadau, Simon Cheyo katibu wa TCCIA wa wilaya ya Kahama na Afisa wa kampuni ya GS1 Tanzania wanaojihusisha na kuweka alama ya utambuzi wa bidhaa , Shabani Mikongoti wamesema maonesho hayo ya kimkakati wa elimu na biashara yatawasaidia sana wawekezaji na wafanyabishara.
Nao baadhi ya wafanyabishara walioshiriki katika kikao na mkuu wa wilaya akiwemo Charles Daud amesema maonesho hayo yatawasaidia sana kuwa na tija kutokana na fursa mbalimbali zitakazotolewa kwa kile alichodai kuwa siku za nyuma walikuwa wamekata tamaa ya kuendelea na biashara.
Mkuu wa wilaya ya Kahama , Festo Kiswaga akielezea kuhusu maonesho ya biashara ya kimkakati ya wawekezaji, wafanyabiashara na wajasiriamali yatakayofanyika Mjini Kahama kuanzia Julai 30,2021 hadi Agosti 8,2021
Source