Sunday, July 18, 2021

Aliyeua na kujiua Dar alikuwa mhasibu chama cha waigizaji




Dar es Salaam. Alex Korosso kwa jina maarufu la Simba anayedaiwa kuua na kisha kujiua, alikuwa mhasibu wa Chama cha Waigizaji Tanzania (TDFAA),imeelezwa.

Hayo yamesemwa leo Jumapili Julai 18, 2021 na mwenyekiti wa chama hicho,Chiki Mchoma maarufu kwa jina la Chiki katika mahojiano yake na Mwananchi.

Tukio la Korosso kujiua lilitokea jana baa ya Lemax maeneo ya Sinza jijini Dar es Salaam, baada ya kuibuka mabishano kati yake na mtu aliyetambulika kwa jina la Gift ambaye alimpiga risasi na kisha naye kujipiga na kufariki hapohapo.

Akimzungumzia Korosso, Chiki amesema alikuwa ni mhasibu wao wa chama baada ya mkutano mkuu wa waigizaji uliofanyika  Mei kumpitisha na kubainisha kuwa katika utendaji wake alikuwa ni mtu mwenye maono katika kukipeleka  chama hicho mbele.


 
"Alex alikuwa mtu mwenye akili nyingi na alikuwa na maono ya kuona chama chetu kikipiga hatua mbele na tayari alishatuandikia madododoso mbalimbali ya kuweza kupata fedha za kukiendesha chama chetu, tumesikitishwa sana na kifo chake," amesema Chiki.

Alipoulizwa kama aliwahi kuwa muigizaji na kaigiza filamu gani, Chiki amesema hakuwa mwigizaji bali alikuwa ni mdau mkubwa wa masuala ya kazi za kuigiza na alikuwa katika mpango wa kuanzisha kampuni yake ya kuandaa kazi za filamu na tayari alishaanza kununua baadhi ya  vifaa.

Kuhusu lini haswa mara ya mwisho kuwasiliana na marehemu, Chiki amesema ilikuwa wiki mbili zilizopita alipokuwa ametoka safarini Uturuki na pia kama siku mbili zilizopita kupitia makundi yao ya Whats App ya viongozi alishiriki katika kutoa mchango wa mmoja wa wanachama wao ambaye anaumwa kwa sasa.


Kuhusu ratiba na wapi msiba upo amesema wanasubiria taarifa za familia yake ambayo ameeleza ipo Moshi mkoani Kilimanjaro.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...