Sunday, July 11, 2021

Abiy Ahmed ashinda uchaguzi kwa kura nyingi Ethiopia




Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ameshinda uchaguzi uliocheleweshwa nchini humo kwa idadi kubwa, bodi ya uchaguzi ilisema Jumamosi.
Bodi ilisema Chama cha Prosperity cha Bw Abiy kilishinda viti 410 kati ya viti 436, ikimpa muhula mwingine wa miaka mitano ofisini.

Walakini, uchaguzi haukufanyika katika baadhi ya sehemu za nchi kwa sababu ya ukosefu wa usalama na shida za vifaa.

Kura hazikufanyika katika eneo lenye vita la Tigray, ambapo maelfu ya watu wanaishi katika hali ya njaa.

Duru nyingine ya uchaguzi imepangwa kufanyika Septemba 6 katika maeneo yaliyoathiriwa, lakini tarehe haijathibitishwa kwa Tigray.

Uchaguzi tayari ulikuwa umecheleweshwa kutokana na janga na Corona hilo.

Bwana Abiy, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, alielezea kura hiyo kama "uchaguzi uliojumuisha watu wengi kihistoria" katika taarifa kwenye Twitter.

Serikali mpya inatarajiwa kuundwa mwezi Oktoba. Walakini, kuna wasiwasi juu ya uadilifu wa uchaguzi.

Vyama vya upinzani vililalamika kwamba ukandamizaji wa serikali dhidi ya maafisa wao ulivuruga mipango yao ya kujiandaa na uchaguzi huo.

Berhanu Nega alisema chama chake, Ethiopian Citizens for Social Justice kilikuwa kimewasilisha malalamiko zaidi ya 200 baada ya waangalizi katika mikoa kadhaa kuzuiwa na maafisa wa eneo hilo na makundi yaliyojihami.

Tume ya Haki za Binadamu ya Ethiopia (EHRC) inayoegemea upande wa serikali ilisema hakuna "ukiukaji mkubwa au wa kuenea kwa haki za binadamu" katika vituo ambavyo iliangalia zoezi la kura.

Walakini, katika ripoti ya awali EHRC ilisema kwamba maeneo mengine yalishuhudia "kukamatwa , vitisho kwa wapiga kura na "unyanyasaji" wa waangalizi na waandishi wa habari'.

Pia ilisema ilikuwa imeshuhudia mauaji kadhaa siku chache kabla ya upigaji kura katika jimbo la Oromia.

Alishinda Tuzo ya Amani ya Nobel ya 2019, lakini mwaka mmoja tu baadaye, alifanya operesheni ya kijeshi katika nchi yake kwa kupeleka wanajeshi katika mkoa wa kaskazini wa Tigray ili kuiondoa TPLF kama chama tawala cha mkoa huo baada ya kuchukua vituo vya jeshi kwa kile Bwana Abiy aliona kama jitihada ya kumwondoa madarakani.

Mzozo huko Tigray umeua maelfu ya watu na kusababisha njaa kubwa .

Jumamosi, kwa mara ya kwanza katika wiki mbili, Shirika la Umoja wa mataifa kuhusu chakula WFP lilianza kuingiza misaada kwenda Tigray. Pande tofauti katika mzozo huo zimekuwa zikituhumiana kwa kuzuia usafirishaji wa misaad kwa raia wanaoihitaji.

Umoja wa Mataifa ulisema Ijumaa kuwa shughuli za kibinadamu zinakwamishwa na kutokuwepo kwa huduma muhimu ikiwa ni pamoja na mafuta, mawasiliano na umeme.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...