CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimesema kimepokea kwa huzuni na masikitiko makubwa kifo cha mwanasiasa mashuhuri aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Kilimanjaro Vicky Nsilo Swai kilichotokea jana Mei 31,2021.
Taarifa ya CCM iliyotolewa na Chama hicho kupitia Katibu wa Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka amesema kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amemtaja marehemu Vicky Nsilo Swai kama mwanasiasa mahiri, mpambanaji, mwenye msimamo thabiti wakati wa uhai wake na alikuwa mstari wa mbele kupigania usawa wa kijinsia, utu na hadhi ya mwanamke.
"Marehemu Mama Vicky ametumia sehemu kubwa ya uhai wake kuwaunganisha Wanawake wa Tanzania na kuwahimiza katika kushiriki shughuli za maendeleo kisiasa, kijamii na kiuchumi, "amesema Rais Samia Suluhu Hassan kupitia taarifa ya Chama hicho
Kwa mujibu wa taarifa ya CCM Vicky Nsilo Swai amewahi pia kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Kilimanjaro. Aidha, akiwa Mke wa Muasisi wa Chama, Marehemu Asanterabi Zephaniah Nsilo Swai, Mama Vicky ameshiriki katika harakati za ukombozi wa Tanganyika pamoja na kusaidia ukombozi wa mataifa mengine kusini mwa Bara la Afrika.
"Miongoni mwa sifa kubwa alizowahi kuwa nazo Marehemu Vicky Swai, ni uaminifu, ambapo amewahi kuhifadhi viatu vya Mpigania Uhuru na Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Afrika Kusini Hayati Mzee Nelson Mandela kwa miaka 33 kuanzia mwaka 1962 vilipoachwa na mpiganaji huyo wa ANC kwa familia ya Mzee Asanterabi Nsilo Swai na kuvikabidhi kwake mwaka 1995 akiwa Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kusini."
Hivyo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa salamu za rambirambi na pole kwa familia ya marehemu Vicky Nsilo Swai na kuwaomba kuwa wavumilivu, wastahamilivu na wenye subira katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wetu.Bwana Ametoa na Bwana Ametwaa, Jina la Bwana Lihimidiwe.