Jeshi la polisi mkoani Mwanza linamshikilia mkazi wa Igoma, Annastazia Kimario (28) kwa tuhuma za wizi wa mtoto mchanga wa miezi mitatu.
Annastazia kimario (28) mkazi wa Igoma jijini Mwanza anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za wizi wa mtoto mchanga mwenye umri wa miezi mitatu kwa nia ya kumridhisha mume wake baada ya kudumu kwenye ndoa muda mrefu bila kupata mtoto.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Muliro Jumanne (anayehamishiwa Kanda maalumu ya Dar es salaam katika mabadiliko yaliyotangazwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Simon Sirro) amesema mtuhumiwa huyo aliiba mtoto huyo Mei 30, mwaka huu katika Kata ya Shibula wilayani Ilemela.
"Mwanamke huyu ambaye ana matatizo ya kupata mtoto alifika nyumbani kwa mama mwenye mtoto na kumuiba baada ya kile alichodai kuwa ni manyanyaso makubwa aliyokuwa akipata kwenye ndoa yake lakini pia kutoka kwa ndugu wa mumewe,"amesema Muliro
Muliro amesema mtuhumiwa alifanikiwa kuiba mtoto huyo baada ya mama mwenye mtoto kumuamini kuwa ni msamaria mwema kwa kujifanya mtu mwenye huruma na kumsaidia kazi mbalimbali ikiwemo kuosha vyombo na kufua nguo za mtoto
Amesema hata hivyo Mei 31, mwaka huu jeshi hilo kwa kushirikiana na kikosi kazi cha sayansi ya uchunguzi lilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo eneo la Kishiri wilayani Nyamagana.
"Mtuhumiwa huyu atafikishwa haraka mahakamani kwakuwa kosa alilolitenda ni miongoni mwa makosa makubwa ya kijinai yasiyovumilika,"
Muliro amewataka wanawake na wanaume wenye matatizo ya uzazi kuwaona wataalamu wa afya ili changamoto zao zipatiwe ufumbuzi badala ya kujenga hisia za kutenda makosa ya kijinai ya wizi wa watoto.
Pia amewaonya wanaume na ndugu wanaoshiriki kunyanyasa wanawake wenye matatizo ya kutopata watoto kwani wanachochea matukio ya wizi wa watoto.
Katika hatua nyingine Kamanda Muliro amewaaga wakazi wa mkoa wa Mwanza na waandishi wa habari akiwashukuru kwakuwa ni sababu ya mafanikio makubwa aliyoyapata wakati akiwa mkoani humo.