Monday, May 3, 2021

Spika Ndugai Amuonya Nape....Atoa Ufafanuzi Sakata La Halima Mdee Na Wenzake

 Spika wa Bunge Job Ndugai leo amesimama bungeni kutoa ufafanuzi wa mambo kadhaa ikiwemo uwepo bungeni wa Wabunge 19 wa Viti Maalum kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo pamoja na kauli alizozitoa Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye kuhusiana na uwepo wa Wabunge hao Bungeni


Spika Ndugai amesema pamekuwa na maneno mengi ya kumshambulia kwenye mitandao ingawa yeye hapendi kushughulika na mambo ya mitandao. 

Ameeleza kuwa wengi wamekuwa wakilisifu Bunge la Tisa lililokuwa chini ya Spika Sitta lakini hawafahamu yeye alikuwa msaidizi wa karibu wa Spika Sitta akihudumu kama Mwenyekiti wa Bunge na ameshiriki kwa kiasi kikubwa katika kutengeneza kanuni za Bunge zinazotumika sasa.

"Mdogo wangu Nape yalimtoka maneno kidogo na yamesambaa sana huko mitandaoni, ikifika mahali Spika na Mbunge mnapishana si jambo jema, yeye ana uhuru wa kusema lakini hana uhuru wa kuwasema wabunge wenzake, nilizungumza nae na ninawaomba mumsamehe, aliwakosea sana na ninaomba sana tuchunge midomo yetu." Alieleza Spika Ndugai

Spika Ndugai amemaliza kwa kuwataka Wabunge 19 wa Viti Maalum CHADEMA waendelee kuchapa kazi huku akisisitiza kwamba ana uzoefu wa kutosha na wanaosema amevunja katiba, hawajui wasemalo kwani yeye hawezi kufanya maamuzi kwa kuandikiwa kipeperushi bali ametaka Katibu wa CHADEMA aandike barua ikiambatanishwa na Katiba ya chama pamoja na muhtasari wa kikao kilichofanya maamuzi.

"Kwa katiba yao chama chao (wabunge 19), Baraza Kuu ndio chombo cha mwisho chenye maamuzi juu ya kufukuzwa kwao. Je, Baraza Kuu limekutana? Je, limefanya maamuzi ya mwisho? Watu wamekata rufaa Baraza kuu, wamesikilizwa? Sasa unawafukuzaje?

"Katibu Mkuu wa chama chochote unapoaniandikia barua juu ya jambo lolote lenye mgogoro, ambao unapelekea mambo ya kikatiba, usiniandikie kipeperushi tu, kwamba mimi fulani, fukuza fulani na fulani. Kazi yangu mojawapo ni kulinda wabunge.

"Nikipata Muhtasari wa kikao cha kuwafukuza (wabunge 19), nitaangalia je hawa wabunge wanaotuhumiwa kufukuzwa walipata nafasi ya kuhojiwa, kusikilizwa na kujieleza?, nifukuze watu ambao hawajasikilizwa kokote?"-Amesema



Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...