NB- Picha haihusiani na habari hapa chini
**
Watu watatu akiwemo Mwenyekiti wa mtaa wa Sanyenge kata ya Old Shinyanga, Benjamin Andrew na waendesha pikipiki wawili wamenusurika kifo baada ya kunyweshwa dawa za miti shamba 'kienyeji' na mtu anayedaiwa kuwa mganga wa jadi kutoka nchini Kenya.
Wakizungumzia tukio hilo leo mchana Jumatano Mei 19,2021 baadhi ya ndugu wa wagonjwa hao wamewataja waliopata madhara kutokana na dawa hiyo kuwa ni waendesha pikipiki Benjamin Godson na Peter Bunzari pamoja na Benjamin Andrew ambaye ni mwenyekiti wa mtaa wa Sanyenge wote ni wakazi wa kata ya Old Shinyanga.
Wakisimulia kuhusu tukio hilo wamesema kuwa awali ndugu zao walikuwa na afya nzuri lakini baada ya kunyweshwa dawa za kienyeji hali zao zilibadilika wakawa wanatoa udenda na mwili kuishiwa nguvu hali iliyowalazimu wawapeleke ndugu zao kituo cha polisi na kisha Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya matibabu.
"Inadaiwa kuwa huyo mganga aliitwa kuja kufichua watu waliovunja duka. Basi leo mchana wanaume wengi walikuwa kijiweni huyo mganga akafika pale na kuwaeleza kuwa ana dawa inaongeza nguvu za kiume. Basi wanaume waakanza kufakamia hiyo dawa, si unajua tena siku nguvu za kiume ni janga!!..Wamepewa dawa kwa gia ya kwamba inaongeza nguvu za kiume ndiyo ghafla watu hao watatu hali zao zilianza kubadilika,wakakosa nguvu",wamesema mashuhuda wakizungumza na Malunde 1 blog.
Inaelezwa kuwa watu hao walikunywa dawa waliyopewa na mganga wa kienyeji kutoka Kenya aliyefika Old Shinyanga kufichua wahalifu waliohusika na wizi kwenye maduka eneo hilo ambapo idaiwa watu wengi eneo hilo walikunywa dawa hiyo hawakupata madhara lakini majanga yakawapata watu watatu pekee.
Kwa upande wao baadhi ya waendesha pikipiki za magurudumu matatu 'Bajaji' waliosafirisha wagonjwa hao wameelezea ilivyo hali ilivyokuwa ngumu kuwasafirisha wagonjwa hao kutoka katika kata ya Old Shinyanga kuwapeleka kituo cha polisi kwani wakiwa njiani katika eneo la Japanise Corner Mjini Shinyanga pikipiki ya kwanza (Bajaji) imepasuka tairi la mbele kisha kuwalazimu ndugu wa wagonjwa kutafuta usafiri wa pikipiki lakini pia Bajaji nyingine (ya pili) baada ya kufika katika eneo la Chuo cha Ualimu Shinyanga (SHY COM) nayo imepasuka tairi la mbele na kuwalazimu kuacha usafiri wa Bajaji na kutumia usafiri wa pikipiki za kawaida.
Mganga mfawidhi wa hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga Dkt. Luzira John amekiri kupokea wagonjwa hao watatu na kwamba wagonjwa wote wamelazwa katika Wodi namba 2 wanaendelea na ya huduma ya matibabu.
Tutawaletea taarifa zaidi kuhusu tukio hili...endelea kutembelea Malunde 1 blog