Serikali ya Korea Kaskazini leo hii imemtuhumu Rais Joe Biden wa Marekani kwa kile ilichokiita kosa kubwa baada ya kuitaja Pyongyang kama kitisho cha usalama katika hotuba yake ya hivi karibuni.
Katika mfululizo wa taarifa zilizochapishwa na shirika la habari la serikali KCNA, taifa hilo limeionya Marekani kwamba itakabiliwa na wakati mgumu sana.
Katika moja ya taarifa hizo mkurugenzi mkuu wa wizara ya mambo ya nje anehusika na mahusiano ya Marekani, Kwon Jong Gun alisema hotuba ya Biden inaonesha wazi dhamira yake ya kuendelea kutekeleza sera ya uhasama dhidi ya Korea ambayo imekua ikitekelezwa na Marekani kwa zaidi ya nusu karne sasa.
Katika hotuba yake ya kwanza ya Jumatano iliyopita kwa bunge la Marekani Biden alisema programu ya nyuklia ya Korea ya Kaskazini inasabisha kitisho cha kiusalama na kwamba inapaswa kushughulikiwa kidiplomasia na kuzuiwa vikali.