Saturday, May 22, 2021

JAFO ATEUA WAJUMBE KAMATI YA USHAURI KUHUSU ELIMU NDANI YA MUUNGANO

1.Mnamo tarehe 17 Mei 2021 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Saidi Jafo (Mb.) aliteua Wajumbe saba (7) kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kwa lengo la kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu uboreshaji wa elimu katika Muungano ili sekta zinazohusika na masuala ya elimu za Tanzania Bara na Zanzibar ziweze kushauriwa ipasavyo. 
 
Hata hivyo kutoka na umuhimu wa Kamati tajwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Saidi Jafo (Mb.) ameongeza wajumbe watatu ili kuongeza ushiriki na upana wa kupata maoni ya pande zote mbili. Kamati hii inaundwa na wajumbe kumi (10), wajumbe watano (5) kutoka Tanzania Bara na wajumbe watano (5) kutoka Zanzibar.

2. Wajumbe walioteuliwa leo ni:-

i. Dkt. Zakia Mohammed Abubakar, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Zanzibar (SUZA)

ii. Prof. Hamed Rashid Hikmany, Mwenyekiti wa Chuo Kikuu cha SUMAIT, Zanzibar na

iii. Prof. Sylvia Temu, Mhadhiri Mwandamizi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

3.    Wajumbe walioteuliwa awali ni:-
 i. Prof. Alexander Boniface Makulilo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Taaluma, Utafiti na Huduma kwa Umma) -         Mwenyekiti

 ii.Mhe. Najma Murtaza Giga (Mb.), Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Viti Maalumu) Zanzibar – Makamu Mwenyekiti
iii.Bw. Abdulmarik Mollel, Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link – Katibu
iv.Bw. Khalid Bakari Hamrani, Mkurugenzi wa Uratibu wa Shughuli za Serikali, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi – Mjumbe
v.Dkt. Charles Msonde, Katibu Mtendaji wa NECTA – Mjumbe
vi. Bw. Gerald Mweli, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI – Mjumbe
vii.Bw. Said Hamad Shehe, Mkufunzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Zanzibar (IPA) – Mjumbe

4.Uteuzi huo umefanyika ikiwa ni hatua ya kushughulikia maoni yaliyotolewa na wadau mbalimbali kuhusu tofauti ya ufaulu wa wanafunzi wa Shule za Sekondari za Tanzania Bara na Zanzibar kwa matokeo mbalimbali ya Kidato cha Nne na Sita. Aidha, Wabunge mbalimbali wamekua wakiwasilisha hoja hiyo wakati wa mjadala wa bajeti ya mwaka 2021/22 wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).

5.    Kamati iliyoteuliwa itafanya kazi kwa siku thelathini na tano (35) na kuwasilisha taarifa kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) ili kwa kushirikiana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi waweze kukaa na Mawaziri wanaohusika na masuala ya elimu kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuwashauri namna bora ya kuboresha elimu pande zote mbili za Muungano.

Lulu Mussa
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini




Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...