Friday, April 9, 2021

Wakuu wa SADC walaani uasi nchini Msumbiji





Viongozi wa mataifa ya Kusini mwa Afrika wametoa taarifa ya pamoja inayoeleezea wasiwasi wao kuhusiana na machafuko ya makundi ya itikadi kali yanayoendelea kaskazini mwa Msumbiji.
Viongozi wa mataifa ya Kusini mwa Afrika wametoa taarifa ya pamoja inayoeleezea wasiwasi wao kuhusiana na machafuko ya makundi ya itikadi kali yanayoendelea kaskazini mwa Msumbiji yaliyosababisha vifo vya maelfu ya watu na wengine wengi kuyakimbia makazi yao. 

Rais wa Botswana, Malawi, Afrika Kusini na zimbabwe walikutana na rais Felipe Nyusi wa Msumbijikatika mji mkuu wa nchi hiyo, Maputo, kuangazia suluhu ya machafuko yanayofanywa na kundi la wanamgambo lenye mafungamano na kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS na kuibua kitisho cha kusambaa machafuko kwenye ukanda huo.

Kulingana na taarifa iliyosambaazwa kwenye vyombo vya habari, wakuu hao wa nchi wameonyesha wasiwasi wao kuhusiana na mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa dhidi ya raia wasio na hatia, wanawake na watoto katika jimbo la Cabo Delgado na kulaani vikali mashambulizi hayo, huku wakithibitisha kwamba mashambulizi mabaya kama hayo hayatakiwi kuendelezwa.

Majengo ya hoteli ambako wakazi na wageni walijificha wakati wa shambulizi katika mji wa Palma. Maandishi yanayoonekana yanaashiria kuomba msaada.

Waasi wenye mafungamano na "Dola la Kiislamu" wadai kuwakata vichwa raia.

Viongozi hao waliokutana ambao ni sehemu ya mataifa 16 ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, SADC wamesema wanataraji kukutana kwenye mkutano mwingine wa kilele utakaojadili mzozo huo Aprili 29, ili kuangazia namna watakavyokubaliana kulishughulikia tatizo hilo kama ukanda. Hata hivyo hakukutolewa maelezo zaidi ya hatua za mapambano dhidi ya ugaidi.

Mkutano huo wa kilele unafanyika siku chache tu baada ya wahanga 12, abao huenda ni raia wa kigeni kukatwa vichwa kufuatia shambulizi lililodaiwa kufanywa na kundi hilo linalojiita Dola la Kiislamu katika mji wa pwani wa Palma uliopo katika jimbo la Cabo Delgado.

Siku moja kabla ya watu hao kukatwa vichwa, rais Nyusi alitangaza kwamba vikosi vya serikali vimerejesha udhibiti wa mji wa Palma baada ya makabiliano na waasi waliokuwa wamejihami kwa silaha.

Zaidi ya waasi 100 waliuvamia mji wa Palma Machi 24. Takriban watu 50 waliuawa kwenye mapigano hayo yaliyodumu kwa siku kumi. Wahanga wengine walikatwa vichwa.

Rais Felipe Nyusi wa Msumbiji amesema pamoja na kuomba msaada, hataki kuuweka rehani uhuru wa taifa hilo.

Maelfu ya watu wameukimbia mji huo, ambao ulikuwa unakaliwa na zaidi ya watu 70,000 kabla ya shambulizi hilo.

Machafuko yatishia mzozo wa kibinaadamu.

Timu ya wataalamu inatarajiwa kupelekwa kaskzini mwa nchi hiyo ili kutathmini hali ilivyo na kupendekeza kuhusu hatua ambazo SADC inaweza kuzichukua.

Akizungumza kwenye mkutano huo, rais Nyusi alikiri kwamba serikali yake iliomba msaada kutoka mataifa mengine, lakini akisema Msumbiji haitaki kuuweka rehani uhuru wake.

Uasi wa kigaidi nchini Msumbiji ulianza tangu mwaka 2017. Na tangu wakati huo, zaidi ya watu 2,600 wameuawa na takriban watu 670,000 wameyakimbia makazi yao, hii ikiwa ni kulingana na Umoja wa Mataifa ambao umeonya kuhusu mzozo mkubwa wa kibinaadamu unaolinyemelea taifa hilo.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...