Ilikuwa tarehe 7 April mwaka 1994 baada ya ndege ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Juvenal Habyarimana ilipotunguliwa akiwa pamoja na aliyekuwa rais wa Burundi Cyprien Ntaryamira.
Kwa mjibu wa umoja wa mataifa watu zaidi ya laki nane, Watutsi pamoja na wahutu wenye msimamo wa wastani waliuawa mnamo kipindi cha siku 100.
Katika kuadhimisha siku hii, inatarajiwa kuwa viongozi wakuu wa serikali wataweka mashada ya maua na kuwasha mwenge kwenye makaburi ya makumbusho ya mauaji ya kimbari eneo la Gisozi mjini Kigali lakini hakuna hafla nyingine zinazotarajiwa kufanyika kutokana na janga la Covid 19.
Wakati huo huo baadhi ya manusura wa mauaji hayo wanalalamikia kutokuwa na makazi huku wengine nyumba zao zikiwa zimezeeka zikihitaji kukarabatiwa.
Shirika linalotetea manusura wa mauaji ya kimbari IBUKA kwa kifupi linasema suala la kutokuwa na makazi kwa manusura linatia wasiwasi wakati huu.
Hata hivyo wakuu wa mfuko wa serikali wa kusaidia manusura wa mauaji ya kimbari wameiambia BBC kwamba swala la makazi hayo litakuwa limeishapatiwa ufumbuzi mnamo miaka miwili kuanzia sasa.Bi Uwacu Julienne ni mkuu wa mfuko huo:
''Manusura ambao bado hawana nyumba ni takriban 870 nchini kote.lengo letu ni kuwa tutakuwa tumekamilisha ujenzi wa nyumba hizo hadi ifikapo mwaka 2024. Na kuhusu kukarabati nyumba za zamani sasa tumeanza sensa ya kujua idadi ya zinazohitaji kukarabatiwa haraka iwezekanavyo''
Mkuu wa mfuko huo anasema kwamba nyumba zipatazo elfu 30 zimekwisha jengwa kwa ajili ya manusura wa mauaji ya kimbari.