Friday, April 9, 2021

Mkurugenzi mtendaji ZLSC awataka Asasi za kiraia kuwa wabunifu


Na Thabit Madai, Zanzibar.

MKURUGENZI mtendaji wa Kituo cha Huduma za Kisheria Zanzibar (ZLSC) Harus Miraji Mpatani amewataka Asasi za kiraia nchini kuwa wabunifu na kutumia njia sahihi katika utatuzi wa migogoro ndani ya jamii. 

Pia amewataka Asasi hizo kujenga mashirikiano na jamii pamoja na Serikali wakati wa utatuzi wa migogoro na majukumu yao ya kila siku  ili kuwa jamii yenye maelewano itakayosaidia kujenga taifa lenye maendeleo endelevu.

Wito huo ameutoa leo wakati akifungua mfunzo ya kuwajengea uwezo Asasi za Kiraia Zanzibar namna ya kutatua migogoro mbalimbali kwa njia ya Amani, Mafunzo hayo ya siku tatu yanafanyika  katika ukumbi wa Kituo hicho cha Huduma na Sheria Kijangwani Mjini Unguja.

Harusi Mpatani alisema kwamba,Asasi za kiraia zina jukumu kubwa katika kushiriki katika utatuzi  wa migogoro mbaimbali inayoikumba jamii hivyo wanatakiwa kuwa wabunifu na kutumia njia sahihi ili kila upande uweze ufaidika.

"Tukiwa kama Asasi za kiraia tunapaswa kuwa waangalifu wakati wa utatuzi wa migogoro, tuwe wabunifu na kujuwa namna sahihi kabisa utatuzi wa hiyo migogoro ili kila upande urizike na usione kama ueonewa, na tusiwe chanzo cha machafuko" alisema.

Aliongeza kwamba, wakati wanapotatua migogoro wanapaswa kuzingatia namna ya kulinda amani ya nchi.

Katika hatua nyingine Harusi Mpatani aliwataka Asasi hio za kiraia kujenga mashirikiano na jamii pamoja na Serikali wakati wa utendaji kazi zao ili kuwa na jamii yenye maelewano na iwe chachu ya kuwa na maendeleo nchini.

Aidha Mkurugenzi huyo akizungumzia Mafunzo hayo aliwaasa washiriki wa mafunzo kusikiliza kwa makini kutoka kwa wakufunzi na kuyatumia katia kazi zao za kila siku kwa maslah mapana ya taifa.

Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na kituo hicho ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa Jenga Amani Yetu unaofadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya na kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Tanzania bara na Zanzibar.

Nae Mratibu na Mkufunzi wa mafunzo hayo Jamila Masoud aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kutumia busara na hekma wakati wa utatuzi wa migogoro katika jamii.

"Unapotumia hekma na busara pamoja na nyenzo mbalimbal tulizo nazo itasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua migogoro kwa njia ya Amani huku pande zote zikiwa zimenufaika," alisema.

Kwa upande wake, Afisa ufuatiliaji na tathimini wa Mradi huo Khamis Haroun Hamad alieleza kwamba, Mradi huo wa miaka miwili kwa Zanzibar unatekelezwa katika visiwa vyote viwili Unguja na Pemba huku Tanzania bara mradi huo ukiwa unatekelezwa na shirika la Search for Common Ground pamoja na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

"Kwa upande wa Tanzania bara mradi huu wa Jenga Amani yetu unatekelezwa na  shirika la Search for Common Ground pamoja na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) katika  maeneo kama vile, Kibiti, Tandaimba, Mtwara na Mara," alieleza.

"Mradi huu walengwa ni makundi mbalimbali katika jamii huku wafadhili wetu ni Umoja wa Ulaya (European Union)," aliongeza kueleza.

Akizungumzia Malengo ya Mradi Khamis alisema kwamba una lengo la kufanya Tanzania kuwa na Amani.

Jumla ya washiriki 25 kutoka Asasi mbalimbali wanapata mafunzo hayo ambayo yanatarajiwa kuedelea siku ya kesho.

 

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...