Na John Walter-Manyara
Mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Manyara Holle Makungu amesema wanamshikilia karani wa mahakama ya mwanzo Magugu Alfred Jackson Ntatirwa kwa makosa ya kuomba na kupokea rushwa kinyume cha Kifungu cha 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa namba 11\2007.
Makungu amesema Ntatirwa anatuhumiwa kwa kuomba rushwa ya shilingi elfu thelathini kisha kukamatwa na maofisa wa Takukuru akiwa amepokea kiasi hicho cha fedha katika mji mdogo wa Magugu wilayani Babati Aprili 6,2021.
Imeelezwa kuwa Mtuhumiwa aliomba rushwa hiyo ili amsaidie mmoja wa wadaiwa kumpatia nakala ya hukumu ambapo mdaiwa hakuwa ameridhika na maamuzi yaliyokuwa yametolewa na mahakama ya mwanzo Magugu hivyo alikuwa na nia ya kukatia rufaa maamuzi hayo.
Hata hivyo karani huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika.
Makungu ameufahamisha Umma wa Wakazi wa Mkoa wa Manyara na Watanzania kwa ujumla kwamba, "Jaji mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mheshimiwa Profesaa Ibrahim Hamis Juma alikwishatoa maelekezo kwa mahakama zote nchini kwamba tangu machi 6,2018 wadaiwa wote hawatalazimika kulipia tozo ya aina yeyote kuhusiana na nakala za hukumu na maamuzi mbalimbali kwa maana ya (Judgements,Rulings,Orders,Decrees and Drawn Ordres)" alisema Makungu
"Maelekezo yanazihusu mahakama kuu,mahakama ya hakimu mkazi, mahakama za wilaya na mahakama za mwanzo. Kwa hiyo ndugu mwananchi ukidaiwa fedha katika hayo niliyoorodhesha fahamu kuwa ni rushwa na unapaswa kutoa taarifa ofisi za TAKUKURU zilizo karibu au kwa kutumia namba yetu ya dharura ambayo ni 113 ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa" Makungu