Tuesday, April 6, 2021

Jay Z awakoroga Waislamu Kenya

 


Mwanamuziki maarufu wa mziki wa Hip Hop wa Marekani Jay Z asababisha hasira miongoni mwa baadhi wa wenyeji wa kaunti ya Lamu baada ya kuonekana amevaa fulana yenye picha ya msikiti wa eneo hilo.


Wenyeji na wawakilishi wa msikiti wa Riyadha ambacho pia ni kituo kinachotoa mafunzo ya dini ya Kiislamu, wameghadhabishwa na mbunifu mmoja nchini Kenya aliyemtengenezea fulana hiyo kwa madai kwamba anatumia vibaya picha ya msikiti wa Lamu.


Hayo yamejiri baada ya Jay Z ambaye pia ni mfayabishara kuonekana akitoka kwenye eneo moja la burudani huko California akiwa amevaa fulana hiyo.


Hata hivyo, usimamizi wa msikiti wa Riyadha umeelekeza hasira zake kwa mbunifu wa fulana hiyo, Zeddie Lukoye, ambaye kampuni yake imekuwa ikielimisha watu kote duniani juu ya historia, asili na taarifa za habari.


Katibu mkuu wa msikiti huo, Abubakar Badawy, alimuandikia barua mbunifu Bwana Lukoye inayomtaka kujitokeza hadharani na kuomba msamaha.


Katika barua hiyo, msikiti huo umeelezea kuwa raia wa eneo wamesikitishwa na picha ya msikiti wao katika kile walichokieleza kama ukosefu wa heshima.


"Hatuchukulii hili kama heshima au pendeleo kwetu kwa msikiti huo wa kihistoria kuoneshwa kwa namna hiyo.


"Baa na vilabu ni kinyume na imani , maadili wala sio heshima kwa msikiti, mwanzilishi wake, umma wake na jamii ya Kiislamu kwa ujumla ndani na nje ya Lamu," Badawy aliandika.


Pia msikiti huo umemtahadharisha mbunifu huyo dhidi ya utumiaji wa tamaduni zingine kuendeleza kitu ambacho ni kinyume na imani yao.


Pia wazee wa Lamu waliomshauri mbunifu huyo kuondoa picha ya msikiti huo miongoni mwa anavyovitangaza na badala yake kutumia nembo nyingine zisizo za kidini kutangaza kaunti hiyo kama vile fukwe za baari,


Msikiti wa Riyadha ni mmoja kati ya misikiti ya kale ambayo bado inatumika kama taasisi ya mafunzo ya Kiiislamu Afrika Mashariki.


Msikiti huo ulijengwa karne ya 19 na pia unatambulika kama urithi wa dunia.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...