Monday, April 12, 2021

Haya Ndio Makaburi ya Kifahari ya Mexico Yanayozidi Ubora Nyumba za Kifahari


Maishani, watu wengi hutaka kuishi katika nyumba nzuri na za kifahari. Wengi huwa hawafanikiwi. Lakini nchini Mexico, ambapo ulanguzi wa mihadarati umekithiri, wakuu wa magenge ya ulanguzi wa dawa za kulevya huishi maisha ya kifahari, na huendeleza hizi hata wanapokuwa wafu.


Nchini humo, utapata makaburi ambayo yangegeuzwa kuwa nyumba, matajiri wengi wangejivunia kuishi.


Ni makaburi makubwa yaliyojengwa na kuwekwa huduma za kisasa na vitu vingi vya anasa.

Kuna baadhi ya makaburi yenye viyoyozi vya kudhibiti viwango vya joto na kuingiza hewa safi, kuna vioo visivyopenya risasi na baadhi yana hata vyumba ambavyo wageni wanaofika kutoa heshima kwa wafu, wanaweza kuketi na kupata kila kitu kinachopatikana katika nyumba za kifahari.



Baadhi yanakadiriwa kugharimu hadi £230,000 (Sh633 milioni za Tanzania; Sh29 milioni za Kenya)


Hali hii ni tofauti kabisa kwa maelfu ya watu wanaouawa katika makabiliano ya magenge ya ulanguzi wa dawa hizo za kulevya ambao sana huzikwa katika makaburi ya pamoja au miili yao kutungikwa na kuachwa ikiwa imening'inia kwenye madaraja.

Ni muongo mmoja sasa tangu serikali ya Mexico ilipotuma wanajeshi wake kwenda kukabiliana na magenge ya walanguzi.


Lakini walanguzi wakuu, ambao wamejipatia pesa nyingi, wanaweza kupamba makaburi yao kutokana na pesa walizolimbikiza kutokana na biashara hiyo.


Makaburi mengi haya hupatikana jimbo la Sinaloa, anamotoka mlanguzi mkuu Joaquin "El Chapo" Guzman ambaye kwa sasa anazuiliwa na anatarajiwa kuhamishiwa Marekani mwakani.



Katika eneo moja la makaburi, Jardines del Humaya, katika mji mkuu wa jimbo la Culiacan, ndipo unapopata baadhi ya makaburi ya kupendeza zaidi.


"Ni ishara ya nguvu na mamlaka ambayo wakati mmoja walikuwa nayo na ni ishara ya matamanio yao ya kutaka kuishi daima, jambo ambalo ni kawaida kwa binadamu yeyote yule," anasema Juan Carlos Ayala, profesa wa falsafa katika chuo kikuu cha Autonomous University cha Sinaloa ambacho huangazia sana utamaduni wa ulanguzi wa dawa.


"Pia ni onesho kwa wale ambao wanaendelea kuishi kwamba mtu huyu alikuwa mtu mashuhuri."


Source
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...