Friday, April 23, 2021

AJICHOMA KISU MARA 12 KIFUANI BAADA YA KUMUUA MPENZI WAKE


Kijana mwenye umri wa miaka 25 anaaminika alijaribu kujitoa uhai kwa kujidunga kisu baada ya kuripotiwa kumuua mpenzi wake huko Kabarnet, Kaunti ya Baringo nchini Kenya. 

Mshukiwa huyo alilazwa katika Hospitali ya Kaunti ya Kabarnet na majeraha mabaya ya kisu.

Jamaa huyo yuko chini ya ulinzi mkali wa polisi kufuatia tukio hilo lililotokea katika kijiji cha Seguton Alhamisi  Aprili 22,2021 jioni. 

Polisi walisema mtuhumiwa huyo alikuwa akiishi na mpenzi wake wa miaka 27 Irene Suke kabla ya tukio hilo. 

Kamanda wa Polisi wa Kaunti hiyo Robinson Ndiwa alisema wapenzi hao wamekuwa wakizozana mara kwa mara katika ndoa yao.

"Tukio hilo la saa 10 jioni liliripotiwa na majirani. Wawili hao walikuwa wamegombana kabla ya kuanza kupigana. Jirani mmoja alikwenda kuchungulia ndani ya nyumba alipowakuta wawili hao wakiwa wamelala sakafuni kwenye damu iliyotapakaa," Ndiwa aliambia The Standard.

 Polisi walipofika eneo la tukio, mwanaume huyo alikuwa amepoteza fahamu huku naye mwanamke akionekana kuwa tayari alikuwa ameaga dunia, Ndiwa aliongeza. 

Mara moja waliwachukua na kuwakimbiza hospitalini ambapo ilithibitishwa kuwa mwanamke huyo kwa jina Suke alikuwa tayari amepoteza maisha yake. 

Ndiwa alisema uchunguzi wa awali ulionyesha kwamba mshukiwa huyo alijidunga kisu kifuani mara tatu kwa kile wanashuku kuwa jaribio la kujiua.

"Mwanaume huyo alikuwa na majeraha 12 ya kisu kifuani na mikononi. Majeraha mikononi mwake yanaonyesha kuwa alikuwa akijaribu kujikinga kutoka kwa mshambuliaji wake, " Ndiwa alisema. 

 Ndiwa aliwashauri wakazi kutafuta njia za kusuluhisha mizozo ya nyumbani ili kuepuka visa vya mauaji.

Daktari katika hospitaliya Kabarnet alisema kuwa mshukiwa anaendelea kupata nafuu ila majeraha yake yalikuwa mabaya. Mwili wa Suke unahifadhiwa katika majkafani ya hospiali hiyo.

 Kisa hicho kinaongeza kwa idadi ya dhuluma za kijinsia katika ndoa ambazo zimeongezeka kwa siku za hivi karibuni hususana kutokana na ugumu wa maisha baada ya mlipuko wa COVID-19 kuripotiwa nchini Kenya.

 Wataalam wanasema kuongezeka kwa visa hivi ni kufuatia mafadhaiko, matukio ya kutatanisha katika mitandao ya kijamii na vile vile hali ngumu ya kiuchumi.

CHANZO - TUKO NEWS

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...