Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Joseph Magufuli amefariki dunia.
Taarifa rasmi iliyotolewa kwa umma na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kupitia Televisheni ya Taifa (TBC) leo usiku Machi 17, 2021 saa 5 usiku imeeeza kuwa Rais Magufuli amefariki dunia leo kwa maradhi ya Moyo akiwa katika Hospitali ya Mzena jijini Dar. Rais Magufuli alilazwa tarehe 6 Machi katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa tatizo la moyo wa mfumo wa umeme.
Nchi itakuwa katika kipindi cha maombolezo kwa siku 14 na bendera zitapepea nusu mlingoti
WASIFU:
Dkt, John Joseph Pombe Magufuli ni mwalimu na mtalaamu wa kemia akiwa na Shahada ya Uzamivu (PhD).
Kuzaliwa
Alizaliwa Oktoba 29 mwaka 1959 huko Chato mkoani Geita, Kaskazini magharibi mwa Tanzania.
Elimu
Magufuli alipata elimu ya msingi katika shule ya msingi Chato kuanzia mwaka 1967 hadi 1974.
Mwaka 1975 alijiunga na Seminary ya Katoke iliyo Biharamulo, Kagera kwa Elimu ya sekondari na kisha kujiunga na shule ya sekondari ya Lake iliyoko Mwanza hadi 1978 alipohitimu.
Mwaka 1979 alijiunga na shule ya Sekondari ya Upili ya Mkwawa, Iringa kwa ajili ya masomo ya kidato cha tano na sita na kuhitimu Mwaka 1981.
Mwaka 1981 hadi 1982 alisomea Stashahada (Diploma) ya Ualimu wa masomo ya Sayansi katika Chuo cha Ualimu cha Mkwawa, Iringa Masomo makuu yakiwa Kemia na Hisabati
Akiwa kazini, Magufuli aliamua kujiendeleza kwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 1985 hadi 1988 alipotunukiwa Shahada ya Ualimu katika masomo ya Kemia na Hisabati.
Mwaka 1991 hadi 1994 alisomea Shahada ya Uzamili ya Kemia (Msc. Chemistry) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Tanzania na Chuo Kikuu cha Salford, Uingereza
Mwaka 2009 alitunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Kemia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Mafunzo ya Kijeshi
Kati ya Mwaka 1983 na 1984, Magufuli alipitia mafunzo ya kijeshi kwa mujibu wa sheria kwenye Kambi za Jeshi la Kujenga Taifa Makutupora - Dodoma, Makuyuni - Arusha na Mpwapwa - Dodoma.
Kazi
Baada ya kufuzu Stashahada ya Ualimu, alifundisha masomo ya Hisabati (Mathematics) na Kemia (Chemistry) katika shule ya Sekondari Sengerema kuanzia mwaka 1983.
Baada ya hapo akafanya kazi kama Mkemia katika Chama cha Ushirika cha Nyanza huko Mwanza hadi mwaka 1995.
Siasa
Nyota ya Magufuli liana kung'aa katika siasa, alipogombea na kushinda ubunge eneo la Chato mwaka 1995. Mwaka huo huo aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, nafasi aliyohudumu hadi Mwaka 2000.
Baada ya uchaguzi Mwaka 2000, aliteuliwa kura Waziri wa Ujenzi, nafasi aliyohudumu hadi Mwaka 2006 alipohamishwa kwenda Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi alipokaa hadi Mwaka 2008.
Mwaka 2010, aliteuliwa kawa Waziri wa ujenzi kwa mara ya pili na kudumu kwenye nafasi hiyo hadi Mwaka 2015.
Urais
Mnamo Tarehe 12 Julai 2015, alichaguliwa kuwa mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Akiwa na Samia Suluhu Hassani kama mgombea mwenza.
Tarehe 29 Oktoba 2015 alitangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushindi wa kura 8,882,935 sawa na 58.46%.
Magufuli aliapishwa kama Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 5 November 2015.
Muhula wa Pili
Mnamo tarehe 30 Oktoba 2020, Tume ya Uchaguzi Tanzania ilimtangaza John Pombe Magufuli kama rais kwa muhula wa pili kwa kupata kura milioni 12.5 hiyo ikiwa ni sawa na asilimia 84 akiwa amemshinda mshindani wake wa karibu, Tundu Lissu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) aliyepata kura milioni 1.9.