Tuesday, March 16, 2021

Naibu Waziri Katambi aagiza kusimamishwa kazi aliyekuwa afisa kazi Mkoa wa Shinyanga





Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughurikia kazi, ajira na vijana Mheshimiwa Patrobas Katambi amemuagiza Katibu Mkuu Ofisi ya waziri Mkuu anayeshughurikia kazi kumsimamisha kazi afisa kazi wa Mkoa wa Tabora bw. Revokatus Mabula anayetuhumiwa kutumia vibaya madaraka yake na kushindwa kufuata maelekezo ya majukumu ya kazi yake.

Naibu Waziri Katambi ametoa maagizo hayo Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kutoa taarifa ya ziara yake katika kanda ya ziwa amesema mtumishi huyo kipindi akiwa afisa kazi Mkoa wa Shinyanga kabla ya kuhamishiwa Mkoa wa Tabora anatuhumiwa kushindwa kusimamia majukumu yake vyema.

Amesema katika ziara yake amebaini kuwa mtumishi huyo alikuwa akiwahujumu wafanyakazi na kuwa upande wa waajiri hivyo kushindwa kusimamia wafanyakazi na haki za wafanyakazi na baada ya kubaini mambo hayo wakati akiwa katika uchunguzi aligundua kuwa jioni ya siku hiyo aliita waandishi wa habari wasitoe habari hiyo.

"Nilitaka kuchukua hatua za papo kwa papo lakini nikataka kujiridhisha zaidi lakini kitu ambacho hakikunifurahisha jioni yake huyu jamaa aliwaita waandishi wa habari kuwataka wasitoe habari hiyo sasa naagiza Mamlaka iliyomteua kumchukulia hatua achukuliwe hatua kali iwe mfano kwa wengine" amesema Katambi.

Amesema katika ziara yake ya kanda ya ziwa amebaini kuwa mgodi wa Elhilal wa Shinyanga kuna baadhi ya wafanyakazi 35 wa mgodi huo kuidai kampuni hiyo mbali na madai hayo pia inadaiwa shilingi milioni 80 za mfuko wa hifadhi ya jamii NSSF kwa watumishi wake.

Naibu Waziri Katambi amesema akiwa katika Mkoa wa Mara katika mgodi wa dhahabu North Mara amebaini udanganyifu mkubwa hasa kwa wageni kufanyakazi bila kuwa na vibali vya kazi jambo ambalo ni kinyume cha taratibu za nchi na kukuta wakifanyakazi ambazo zingeweza kufanywa na watanzania huku taarifa ikionyesha kazi hizo zinafanywa na wazawa.

"kulikuwa na udanganyifu mkubwa kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama tuliweka mtego na kubaini raia wa kigeni wakifanyakazi ambazo zingefanywa na wazawa na tukafanikiwa kumnasa raia wa kigeni akifanyakazi za manunuzi na huduma za malipo na kubaini wapo wengene tisa (9) kufanyakazi bila kuwa na vibali" amesema.

Amesema mbali na mapungufu hayo amebaini kuwa kuna kampuni ndogo zinazofanyakazi na mgodi huo zimekuwa na udanganyifu mkubwa sana kwa mfano kampuni ya Kiribo kushindwa kulipa wafanyakazi zaidi ya milioni 300 na kukwepa kulipa kodi na fedha za mifuko ya hifadhi ya jamii hadi kufikia bilioni 1.1 na kodi ya shilingi bilioni 1 ambazo zingelipwa kwa Serikali.

Ameagiza mamlaka za Mkoa wa Mara kumfikisha Dodoma uongozi wa mgodi huo na  mmiliki wa Kampuni hiyo kwa ajiri ya kufanya maongezi ili kuweza kulipa madai hayo na kulipa kodi ya Serikali na uzoefu unaonyesha kuwa kampuni kama hizo zimekuwa zikitengeneza migogoro na kupotea na serikali inashindwa imuadhibu yupi kwa makosa hayo.

Pia Naibu Waziri Katambi amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Mfuko wa hifadhi ya jamii NSSF Bw. William Erio kuwasimamisha kazi Mkurugenzi wa NSSF Mkoa wa Mara Bw. Maneno Mpogole na Abdulabi Salehe kwa kutotimiza majukumu yao kwa kushindwa kudai madeni kampuni hiyo hadi deni kufikia bilioni 1.1 huku ikionyesha fedha hizo zilikuwa hazifuatiliwi.

Amesema wasimamishwe kazi ili uchunguzi ufanyike ni kwanini fedha hizo hazikufuatiliwa hadi kufikia bilioni 1.1 na kutoa onyo kwa mameneja wengine wa Mikoa kufuatilia madeni wanayodai kwenye taasisi za binafsi na za Serikali kuhakikisha madeni yanakusanywa kwa mujibu wa sheria.

Aidha kutokana na kuwepo kwa udanganyifu katika vibali vya kazi ameagiza maombi yote ya vibali yaombwe kwa kamishna wa kazi ili kuepuka vishoka ambao wamekuwa wakidanganya kuwa wanauwezo wa kuwatafutia vibali vya kazi na mwisho kuishia kuwatapeli tu.

Kwa upande wake Kaimu Kamishna wa kazi Andrew Hebron ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Serikali sambamba na kutoa vibali vya kazi kwa wakati kwa wageni wanaoomba vibali vya kazi.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...