WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itatekeleza mikakati mahususi ya kuongeza ukusanyaji wa mapato ambayo ni pamoja na kukasimisha jukumu la kukusanya kodi ya majengo kwa Halmashauri na Serikali za Mitaa.
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali itaimarisha ushirikiano kati ya mamlaka zinazokusanya mapato na vyombo vya ulinzi na usalama katika kufanya doria maeneo ya mipaka ya nchi kavu, baharini na kwenye maziwa ili kudhibiti biashara za magendo.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumamosi, Februari 13, 2021) wakati akiahirisha Mkutano wa Pili wa Bunge la 12, Bungeni jijini Dodoma. "Pia Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi kwa kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wote wanatumia mashine za kutolea risiti za kielektroniki (EFD)."
Kuhusu mikopo ya elimu ya juu, kwa mwaka huu 2020/2021 Waziri Mkuu amesema Serikali imetoa mikopo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza 55,287. Pia itaendelea kuzingatia kigezo pekee cha uhitaji wa mwombaji sanjari na kurahisisha matumizi ya mtandao katika uombaji na utoaji wa mikopo.
Amesema katika kuongeza ufanisi wa utoaji na urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu, Serikali imefanya maboresho ya kisheria, kimfumo na kiutendaji kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita (2015/2016 – 2019/2020).
Waziri Mkuu amesema matunda ya maboresho hayo ni pamoja na kuongezeka kwa makusanyo ya fedha za mikopo kutoka wastani wa shilingi 28.9 bilioni mwaka 2016/2017 hadi kufikia wastani wa shilingi 192 bilioni mwaka 2019/2020.
"Serikalini inafarijika na inapokea kwa mikono miwili michango yenye afya na tija kuhusu hatma ya mikopo inayotolewa na Serikali baada ya miaka 15 ya uwepo wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu na ipo tayari kuendelea kujifunza kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote nchini kuhusu namna bora zaidi ya kuufanya mfuko huu."
Amesema ili mfuko huo uwe endelevu na himilivu na wenye manufaa katika ujenzi wa uchumi wa Taifa, ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kushirikiana na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ili kuboresha huduma zake na kurahisisha urejeshwaji wa mikopo kwa wanufaika waliojiari katika sekta binafsi.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi wanufaika wote wa mikopo ya elimu ya juu, ambao bado hawajajitokeza na kuanza kurejesha, wafanye hivyo mara moja, pia amewataka waajiri wote nchini katika sekta binafsi na sekta ya umma, watoe kipaumbele kwa makato ya mikopo ya elimu ya juu kama yalivyo makato mengine ya kisheria