Saturday, February 6, 2021

Watatu Azam kuukosa mchezo dhidi ya Simba kesho

 


Ligi kuu soka Tanzania bara inatazamiwa kuendelea tena siku ya kesho Jumapili, Februari 7, 2021 kwa michezo miwili ya viporo, Simba kukipiga na Azam saa 10:00 jioni, wakati huo huo Namungo watawakaribisha Maafande wa Ruvu Shooting kwenye dimba la majaliwa mkoani Lindi.


Kuelekea kwenye mchezo wa Simba dhidi ya Azam utakaochezwa kwenye dimba la mkapa jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya Habari na mawasiliano wa klabu ya Azam, Zakaria Thabiti 'Zaka zakazi' amethibitisha kuwa watawakosa nyota wake watatu kwasababu mbalimbali.


Wachezaji watakaokosekana ni mlinzi wa kati, raia wa Ghana,Yakubu Mohamed anayetumikia adhabu ya kukosa mchezo mmoja baada ya kuoneshwa kadi za njano tatu, kiungo Frank Dumayo mwenye maumivu ya goti yatakayo muweka nje ya uwanja kwa muda wa mwezi mzima.


Mchezaji watatu atakayekosekana ni mlinzi wa kulia chaguon la pili, Abdul Omary Hamahama mwenye majeraha ya mguu ambaye anatazamiwa kurejea baada ya majuma kadhaa.


Licha ya wachezaji hao kuthibitishwa kuwa watakosekana kwenye mchezo huo mkubwa dhidi ya bingwa mtetezi wa VPL, kocha mkuu wa Azam, George Lwandamina huenda asiumize kichwa sana kutokana na kuwa na wachezaji wazoefu wakikosi cha kwanza wanaoweza kuziba nafasi hizo.


Mlinzi wa kati, Abdallah Heri 'Sebo' huenda akapangwa kucheza na Daniel Amoah ama mkongwe, nahodha wao Aggrey Moris wakati kwenye eneo la kiungo, Mudathir Yahya huenda akachukua nafasi ya Domayo na mlinzi bora wa VPL na mchezaji wa Uganda, Nicolas Wadada akacheza mlinzi wa kulia


Uongozi wa Azam kupitia Afisa mtendaji wake, Abdulkarim Amin 'Popat' wamejinasibu kuchukua alama tatu muhimu kutokana na maandalizi mazuri waliyoyafanya wakati huo huo kocha msaidizi wa Azam, Bahati Vivier amesema wataingia uwanjani kuwaheshimu Simba lakini wanawinda ushindi tu.


Azam ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi wakiwa wamecheza michezo 17 na kujikusanyia alama 32 utofauti wa alama 6 na Simba waliopo nafasi ya pili na utofauti wa alama 12 na vinara wa lgii hiyo klabu ya Yanga.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...