Chama tawala nchini Chad leo kimemuudhinisha rais Idriss Deby kuwania muhula wa sita katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Deby amesifu uamuzi huo wa chama chake cha PSM na amesema baada ya kutafakari kwa muda mrefu ameridhia kupeperusha tena bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi unaokuja.
Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 68 ambaye ameitawala nchi hiyo kwa miaka 30 anatarajiwa kuchuana na kiongozi wa muungano wa upinzani katika uchaguzi huo wa April.
Licha ya kuiongoza Chad kwa mkono wa chuma, Deby anaungwa mkono na jumuiya ya kimataifa inayomuona kuwa mshirika muhimu kwenye mapambano dhidi ya makundi ya itikadi kali kwenye kanda ya Sahel.
