MWENYEKITI wa klabu ya Namungo, Hassan Zidadu amesema wachezaji watatu na kiongozi mmoja wa klabu hiyo waliokwama nchini Angola baada ya kukutwa na maambukizi ya Covid-19 wameachiwa huru na tayari wameshaanza taratibu za kuwarudisha nchini.
"Tulikuwa tunawasiliana nao kila siku, asubuhi, mchana na jioni. Lakini serikali ya Angola ilisema itawaachia wakiwapima na kujiridhisha kama hawana maambukizi. Tunashukuru Mungu kwa mujibu wa vipimo vyao jana asubuhi na majibu kutoka mchana, hawana maambukizi na wameachiwa huru".
"Tunasikitika kwasababu serikali ya Angola iliahidi gharama za kuwasafirisha lakini leo imejitoa na badala yake inabidi sisi tuwasafirishe wenyewe na tumeshaanza utaratibu huo. Watarejea nchini kati ya Jumamosi au Jumatatu".
Ikumbukwe, Wanne walikutwa na maambukizi wakati Namungo ilipowasili nchini Angola kwa ajili ya kucheza dhidi ya Premiero de Agsoto ya nchini humo kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa mtoano kuwania kufuzu hatua ya makundi ya kombe la shrikisho barani Africa.
Baada ya Skata hilo, Shirikisho la soka barani Afrika 'CAF', liliamua kuufuta mchezo huo na siku chache baadaye ukapangwa uchezwe nchini Tanzania. Wawili hao wamekipiga siku ya Jumapili ya tarehe 21 Februari mwaka huu katika dimba la Chamazi na Namungo kuibuka na ushindi wa mabao 6-2 ikihesabiwa kama mchezo wa ugenini dhidi ya timu hiyo ya nchini Angola.
Mchezo wa mkondo wa pili wa wawili hao, unataraji kupigwa leo tarehe 25 Februari saa 11:00 jioni kwenye dimba la Chamazi jijini Dar es Salaam, Namungo akiutumia uwanja huo kama dimba lake la nyumbani. Kuelekea kwenye mchezo huo, Mwenyekiti wa Namungo Zidadu amesema maandalizi yamekamilika kwa 95% hivyo wanasubiri muda ufike waumalize mchezo.
"Maandalizi yamekamilika kwa 95% kila sekta, benchi la ufundi na wachezaji wamefanya mazoezi yakutosha. Safari hii tunachezea kwenye uwanja wa Chamazi wa Azam Complex, uwanja unaotupenda kwani hatujawahi kupata matokeo mabaya".
"Maeneo mengine yote yapo sawa sawa, tunasubiri muda ufike tuingie kwenye eneo la kuchezea".
Endapo Namungo ikitoka sare ya aina yeyote au kupata ushindi basi itafuzu kucheza hatua ya makundi ya michuano ya kombe la shirikisho kwa mara ya kwanza tokea kuanzishwa kwa klabu hiyo na itacheza kutoka kundi D lenye, Pyramids ya Misri, Raja Casablanca ya Morocco na Nkanza ya Zambia.
Ili Primeiro de Agosto ya Angola iweze kufuzu basi inahitaji ushindi wa utofauti wa kuanzia mabao 5 na kuendelea.