Mbunge wa Ulyankulu (CCM), Rehema Migila amesema shule ya sekondari ya Isike iliyopo kata ya Igombe mkoani Tabora nchini Tanzania imegeuka makazi ya ngedere na nyani baada ya kufungwa.
Migila amezungumza hayo leo Jumanne Februari 2, 2020 bungeni mjini Dodoma wakati akiuliza maswali ya nyongeza.
Mbunge huyo amesema baada ya kufungwa kwa shule hiyo, idadi ya wanafunzi imekuwa kubwa katika shule ya sekondari Ulyankulu na kusababisha wengine kuhamishiwa shule ya sekondari ya Mkindo ambayo siyo ya bweni.
Amehoji Serikali haioni haja ya kuwarudisha wanafunzi katika shule ya Isike ambao wanatembea umbali mrefu na kuwaongezea wazazi gharama.
"Shule ile imefungwa sasa hivi haifanyi kazi yoyote ile imekuwa makazi ya ngedere na nyani hali ambayo inasababisha wananchi usumbufu na Serikali ilitupa nguvu bure na raslimali fedha pasipokuwa na maana," amesema.
Akijibu maswali hayo waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo amesema kwa kuwa mbunge ndiye yupo katika eneo husika ndio anajua mahitaji na kumuagiza ofisa elimu wa Mkoa wa Tabora kufanya tathmini na kuleta majibu haraka katika shule hiyo ili kuwasaidia watoto wa eneo hilo.