Wednesday, February 10, 2021

Mapya yaibuka madaktari wanaoikimbia serikali

 


Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel, amesema kuwa kwa sasa wanaompango wa kudhibiti watumishi wa sekta ya afya walioajiriwa na serikali lakini wanafanya kazi kwenye sekta binafsi ili kuhakikisha huduma serikalini zinaimarika na kukuza mapato.


Kauli hiyo ameitoa hii leo Februari 10, 2021, Bungeni Dodoma, wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalum mkoa wa Tanga, Mwantumu Zodo, lililohoji serikali imejipanga vipi kuhakikisha huduma za afya kwenye vituo vya afya vya serikali ikilinganishwa na sekta binafsi.


"Wizara ya Elimu wanashirikiana vizuri sana na sekta binafsi bila kuwepo anayenyonywa upande mmoja, lakini kwenye afya tutaenda kudhibiti hasa kwenye eneo la kwamba unakuta kuna watumishi wa kufanya kazi serikalini wako eneo la private sector wakati wameajiriwa serikalini nalo hili litafanyiwa kazi kwa nguvu" , amesema Dkt. Mollel.


Ikumbukwe kuwa mapema mwaka huu wakati Rais Dkt. Magufuli, akizindua jengo la wagonjwa wa dharura katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tabora Kitete, alimwagiza Waziri wa Afya, Dkt. Dorothy Gwajima, kuhakikisha anawafuatilia madaktari wote ambao waliajiriwa na serikali na kisha kuacha kazi na kukimbilia sekta binafsi.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...