Monday, February 22, 2021

Maombi kupambana na corona yaanza Moshi


Waumini wa Jimbo katoliki la Moshi leo Februari 22, 2021 wameanza maombi maalum ya saa 48 mfululizo kwa ajili ya kumwomba Mungu alinusuru Taifa na ulimwengu kwa ujumla na janga la corona.


Ombi hilo lilitolewa  Februari 11, mwaka huu na Askofu wa jimbo hilo, Askofu Ludovick Minde ambapo amewataka mapadre, watawa na waumini wote walei wa jimbo hilo kufanya sala hiyo kwa imani wakiamini kwamba Yesu wa Ekaristi hashindwi kamwe katika jambo lolote jema.


"Tuingie kwa nia moja kwa juhudi kubwa katika kipindi hiki maalumu cha sala, iwe wazi na dhahiri kabisa kwamba ni jimbo lote la Moshi, katika ujumla wetu tupo chini ya miguu ya  Yesu kwa unyenyekevu mkubwa tukimwomba azinusuru familia zetu, kanisa na ulimwengu mzima kwani tunaangamia,"Askofu Minde


Alisema kutokana na hali halisi ya ugonjwa wa corona ambao unatikisa familia, wahudumu wa kanisa na ulimwengu kwa ujumla ni wakati sasa wakumlilia Mungu kwa nguvu zote ili aepushe ugonjwa huu.


"Tukiwa tumejawa na mahangaiko makubwa, huzuni na maumivu ya ndani na nje kwa mioyo iliyojaa imani, matumaini, upendo na unyenyekevu mkubwa kwa Mungu, tumeamua tena kumkimbilia kwa namna ya pekee kabisa tukimwomba na kumsihi kabisa atunusuru katika hali hii mbaya,"


Maombi hayo ambayo yameanza leo yatahitimishwa Februari 24, mwaka huu kwa misa takatifu na baraka ya sakramenti kuu katika maeneo yote yaliyotajwa.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...