Kocha Dylan Kerr, amesema kikosi cha Simba SC kina uwezo mkubwa wa kuifunga Al Ahly kwenye mchezo wa kesho Jumanne, ambao utachezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Kocha huyo ambaye aliwahi kukinoa kikosi cha Simba SC akisaidiana na Seleman Matolla msimu wa 2015–2016, amesema Al Ahly ina kikosi cha kawaida kama ilivyo kwa vikosi vya klabu nyingine barani Afrika, hivyo suala la kufungwa ni la kawaida pia.
Kocha huyo raia wa Malta ambaye kwa sasa anafanya kazi Afrika Kusini akiwa na klabu ya Baroka FC amesema, anaamini Simba SC itakua na wakati mzuri kesho, ikiwa itacheza soka la ushindani na kutumia nafasi itakazozipata.
Pitso Mosimane: Tupo tayari kwa mchezo, hakuna la kuhofia
"Huwa nasema kwa michezo ya nyumbani Simba inahitaji kufunga inapopata nafasi, timu ya Pitso Mosimane ina sifa nzuri lakini ugenini huwa wanapigwa kila wakati."
Kerr, ambaye baada ya kuondoka Simba SC alijiunga na Gor Mahia ya Kenya na kuitumikia kuanzia 2017–2018, pia amewataka mashabika wa Wekundu hao wa Msimbazi kufika Uwanja wa Benjamin Mkapa bila kukosa ili kuipa nguvu timu yao, ambayo itakua na kazi ya kusaka ushindi nyumbani dhidi ya Al Ahly.
"CAF imeruhusu mashabiki 30,000 kuhudhuria mchezo huo, mashabiki wanapaswa kufika uwanjani bila kukosa, ninaamini kama mashabiki watafika uwanjani na kushangilia kwa nguvu, hakika timu ya Simba SC itafanya vizuri dhidi ya Al Ahly,"
Simba SC: Tutaikalisha Al Ahly kwa Mkapa
"Mashabiki wa Simba ni wa kushangaza sana, hawakati tamaa, wanaunga mkono timu yao kutoka mwanzo hadi filimbi ya mwisho, najua watawasaidia wachezaji wao." Amesema Kerr alipohojiwa na Goal.Com
Simba SC na Al Ahly wanakutana katika mchezo wa mzunguuko wa pili wa Kundi A kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kesho Jumanne (Februari 23), huku kila mmoja akiwa na kumbukumbu ya kushinda mchezo uliopita.
Simba SC ilishinda mchezo wake wa kwanza kwa bao 1-0 ugenini dhidi ya AS Vita Club ya DR Congo wakati Al Ahly ambao ni mabingwa watetezi, iliifunga Al Merrikh ya Sudan mabao 3-0 mjini Cairo.