Tuesday, February 23, 2021

Dk. Mpango: Nililetwa hospitali na mtungi wa Oksijeni


DAKTARI Philip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania, ameeleza namna alivyokabiliana na tatizo la upumuaji, kwamba alifikishwa hospitali akiwa na mtungi wa gesi ya Oksijeni. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Ametoa kauli hiyo mbele ya waandishi wa habari katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma leo Jumanne tarehe 23 Februari 2021.

"Nimekaa hapa (Hospitali ya Benjamin Mpaka) siku 14 na nilikuja hapa na mtungi wa Oksijeni, na leo ni siku ya tatu sijawahi kutumia mtungi wa Oksijeni. Nataka kuwaambia Watanzania, afya yangu imeanza vizuri kabisa."


 
"Siku 14 nilizokuwa nahudumiwa nyumbani na baadaye madaktari wakaamua kunihamishia hapa (hospitalini), tumtukuze Mungu, mwacheni aitwe Mungu. Namshukuru Mungu kwa kunipa nafasi nyingine," amesema Dk. Mpango, ambaye ameruhusiwa kutoka hospitalini

Dk. Mpango ameshauri Watanzania kumwomba Mungu awavushe wagonjwa wengine kama ambavyo amevushwa yeye.


Amesema, ameona upendo wa Watanzania katika kipindi ambacho alikuwa akipatiwa matibabu huku akiwashukuru manesi na madaktari kwa juhudi zao.

"Nimeonja upendo mkubwa kwa wananchi wa Tanzania na wananchi wenzangu wa Buhigwe, wawe na amani na muda si mrefu nitakwenda kuwatembelea.


"Madaktari, manesi, wataalamu wa viungo, mpaka wahudumu nawashukuru sana kwa huduma nzuri mlizonipa katika kipindi chote. Ni vijana lakini wanafanya kazi kubwa sana," amesema Dk. Mpango.

Amesema, wakati akipatiwa matibabu, alikuwa akishawishiwa kuhamishiwa Dar es Salaam ili apate huduma bora zaidi.


Hata hivyo, amesema Hospitali ya Benjamin Mkapa ni bora na ina huduma nzuri, na kwamba alipingana na ushawishi huo.

"Kulikuwa na vishawishi 'hamia Dar es Salaam, hamia huku' nikasema, hapana, hospitali ni nzuri kabisa na wataalamu walioiva.


Dk. Philip Mpango, wakati akiwa Waziri wa Fedha na Mipango 2015-19
"Sababu ya kukimbilia Ulaya, haipo. Tuboreshe vya kwetu na kwa nafasi aliyonipa rais, nitamshauri kuboresha zaidi. Natoa pole sana kwa familia ambazo zimepoteza wapendwa wao kwa wiki mbili ambazo nimekuwa hapa na wiki mbili nikiwa nyumbani," amesema.

Ameeleza kutamani kushiriki katika baadhi ya misiba ikiwa ni pamoja na wa Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais visiwani Zanzibar uliotokea wiki iliyopita, lakini pia msiba wa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi.

"Ningeshiriki msiba wa Maalim Seif na Balozi John Kijazi, na jana nimempoteza mwalimu wangu wa pekee, Profesa Benno Ndulu (Gavana Mstaafu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na mdogo wangu Atashasta Nditiye (aliyekuwa Mbunge wa Muhambwe).

"Natoa sana pole kwa familia kwa kuondokewa na wapendwa wao na nikipata nafasi, nitaona fursa ya kushiriki hapo baadaye," amesema.

Dk. Mpango amesema, anarejea kazini, na kwamba tayari ameanza kazi ndogondogo za kulitumikia Taifa.

"Watanzania tuendelee kumwomba Mungu kwa kila mmoja na imani yake na atatuvusha. Amenivusha mimi na wengine ninaowaacha hapa atawavusha," amesema.


 


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...