Mahakama ya juu nchini Burundi imeweka hadharani kwa mara ya kwanza hukumu ya kifungo cha maisha jela ya majenerali wa zamani wa jeshi la taifa hilo, wanasiasa , waandishi na wanaharakati kwa jaribio la mapinduzi yaliofeli 2015, hati za mahakama zinasema.
Jaribio la mapinduzi hayo lilitokea baada ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, marehemu Pierre Nkurunziza kutangaza kusudio la kugombea urais kwa kipindi cha tatu, jambo lililopingwa na baadhi ya wanachama wa CNDD-FDD na kusababisha machafuko yaliyosababisha vifo, majeruhi na baadhi ya wananchi kukimbilia nchi za jirani.
Katika hukumu hiyo iliyotangazwa hivi karibuni, watu hao 34 wametangazwa kuwa na hatia na kutakiwa kulipa faini ya dola za Marekani 780,000 kwa waathiriwa wanaohusishwa na chama tawala cha CNDD-FDD.
Miongoni mwa waliohukumiwa ni pamoja na Jenerali Godefroid Niyombare aliyeongoza jaribio hilo la mapinduzi, Potien Gaciyubwenge aliyekuwa Waziri wa ulinzi na Leonidas Hatungimana ambaye alikuwa msemaji wa Rais Nkurunziza.
Wengine ni pamoja na aliyekuwa makamu wa rais Bernard Busokoza, OnesimeNduwimana, mkosoaji mkubwa wa serikali Marguerite Barankitse, mwanachama wa upinzani anayeishi Ulaya na waandishi wa habari waliokuwepo wakati huo wa mapinduzi.
Hata hivyo, kesi hiyo imechukuliwa kama mwendelezo wa madai ya kuwapo kwa chuki katika Serikali ya Burundi.
''Kesi ya kundi moja la watu ambayo haionyeshi jukumu la kila mmoja wao huku ikiwa hakuna hata mshukiwa mmoja aliyehudhuria, ni kesi ya chuki na maamuzi ya kisiasa ambayo yalipatiwa majaji kutia saini'', alisema Onesime Nduwimana alipohojiwa na Shirika la Habari la Uingereza (BBC).
Naye Bob Rugurika ambaye ni mwandishi na mkurugenzi wa redio ya kibinafsi iliyopigwa marufuku nchini humo na ambaye naye pia amehukumiwa katika kesi hiyo, ameandika katika ukurasa wake wa Twitter akisema:
''Ni vigumu, lakini hatutakubali iendelee hivyo."
