Sunday, January 3, 2021

Sudan, Ethiopia na Misri kufanya mazungumzo mapya juu ya bwawa la mto Nile


 Sudan itashiriki kwenye duru mpya ya mazungumzo na Misri na Ethiopia yatakayofanyika hii leo Jumapili. 

Mazungumzo hayo yanalenga kuutatua mgogoro wa muda mrefu juu ya bwawa kubwa la kuzalisha umeme linalojengwa na Ethiopia kwenye Mto Nile. 

Nchi hizo tatu zimefanya duru kadhaa za mazungumzo tangu Ethiopia ilipozindua mradi huo mkubwa mnamo mwaka 2011, lakini bado hazijafaulu kufikia makubaliano kuhusu kujazwa maji kwenye bwawa hilo pamoja na utendaji kazi wake. 

Mazungumzo yaliyofanyika kwa njia ya video mwezi Novemba, yalivunjika bila kufikiwa hatua yoyote. 

Shirika la habari la Sudan - SUNA limesema maafisa kutoka Afrika Kusini ambayo ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, watashiriki katika duru hiyo mpya ya mazungumzo. 

Umoja wa Ulaya ambayo ni miongoni mwa waangalizi wa mazungumzo hayo umesema mazungumzo hayo yanatoa fursa nzuri ya kupigwa hatua katika kufikia muafaka.



Source
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...