Friday, January 22, 2021

Mkazi wa Babati ahukumiwa maisha jela kwa kumbaka mtoto


Na John Walter-Babati

Mkazi wa Babati mkoani Manyara  anayejulikana kwa jina  Isaya Faustine mwenye umri wa miaka 23, amehukumiwa kutumikia kifungo cha maisha jela baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 10.

Hukumu hiyo imetolewa katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Manyara ,mbele ya hakimu Mheshimiwa Simon Kobelo baada ya kujiridhisha na ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo.

Mahakama ilieleza kuwa Mshtakiwa alifanya kosa hilo la kubaka Novemba 23,2019 katika Kesi hiyo namba 35 ya mwaka 2020 ambapo ni kinyume na kifungu cha 130 na kifungu kidogo cha 1 na cha 2 (E).

Kwa upande wake Wakili wa Serikali  Roda Kisiye  aliitaka mahakama kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa ili iwe fundisho kwa jamii.

Wadau wa masuala ya ukatili wa jinsia mkoa wa Manyara wamepongeza uamuzi wa mahakama kwa kueleza kuwa  unalenga kulinda haki na ustawi wa watoto katika jamii.

Mkuu wa dawati la jinsia Polisi mkoa wa Manyara Pili Saburi amewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa ya matukio ya ukatili unaofanywa katika maeneo yao ili vitendo hivyo viweze kukomeshwa.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...