Maandamano yamezuka leo katika zaidi ya miji 60 ya Urusi kudai kuwachiliwa huru kwa kiongozi wa upinzani Alexei Navalny, ambaye ni mkosoaji mkubwa wa serikali ya Urusi. Polisi wa Urusi wamewakamata zaidi ya waandamanaji 1,000.
Mjini Moscow, karibu waandamanaji 5,000 waliujaza uwanja wa Pushkin katikati mwa mji huo mkuu, ambako makabiliano yalizuka na waandamanaji wakaburuzwa na askari wa kutuliza na ghasia hadi kwenye mabasi ya polisi na kuzuiliwa kwenye malori. Mke wa Navalny, Yulia Navalnaya ni miongoni mwa waliokamatwa.
Maandamano hayo yalishuhudiwa katika maeneo mengi ya Urusi kuanzia mji wa kisiwa wa Yuzhno-Sakhalinsk kaskazini mwa Japan na mji wa mashariki mwa Siberia wa Yakutsk ambako baridi kali limetanda, mpaka miji mingine ya Urusi yenye watu wengi katika upande wa Ulaya.
Ukubwa huo wa maandamano unaashiria jinsi Navalny na kampeni yake ya kupambana na rushwa walivyojenga mtandao mpana ya uungaji mkono licha ya ukandamizaji rasmi wa serikali na kupuuzwa kila mara ya vyombo vya habari.
