Na Ahmad Mmow, Lindi.
Miongoni mwa sababu za timu za soka mjini Lindi kushindwa kuwa imara imetajwa kuwa ni tofauti za itikadi za vyama vya siasa.
Hayo yalielezwa jana na Mbunge wa Lindi mjini, Hamida Abdallah baada ya kukabidhi msaada wa fedha taslimu shilingi 600,000 kwa timu ya soka ya Lindi United FC. Hafla ambayo ilifanyika katika ukumbi wa Double M, manispaa ya Lindi.
Mbunge Hamida alisema miongoni mwa sababu zinazosababisha timu za soka za wilaya ya Lindi kushindwa kudumu na kufanya vizuri ni tofauti za itikadi za siasa kuingizwa kwenye michezo.
Alisema hali hiyo inawakatisha tamaa wadau wa michezo wenye nia njema ya kuzisaidia timu hizo. Kwani wanaogopa kunasibishwa na vyama vya siasa. Hivyo kusababisha kusiwe na timu imara katika wilaya hiyo, hasa manispaa ya Lindi.
" Mimi leo nimekuja hapa kutoa mchango wangu, ni miongoni mwa ahadi ambazo niliahidi wakati wa kampeni. Pia ilani ya chama changu (CCM) imezungumzia suala la michezo. Nimekuwa nikisaidia timu mbalimbali tangu nikiwa Mbunge wa viti maalumu. Nilisaidia vifaa vya michezo takribani timu kumi na sita, lakini sio ajabu kesho tu tutasikia Lindi United ni timu ya Chama Cha Mapinduzi," alisikitika Hamida.
Kwakuzingatia ukweli huo amatoa wito kwa viongozi wa timu hiyo ambayo ni bingwa wa soka wa mkoa wa Lindi kutoihusisha na itikadi za siasa. Kwani wadau wa soka wana itikadi tofauti za vyama vya siasa. Kwahiyo wasipokuwa makini wanaweza kukosa misaada kutoka kwa wadau ambao hawapendi mambo ya siasa.
Aidha alitoa wito kwa viongozi wa timu za soka ambazo ni mchezo unaopendwa na watu wengi, wabuni miradi ya uchumi itakayoingiza mapato kwa timu zao badala ya kutegemea misaada. Maana siyo watu wengi wenye moyo wa kusaidia.
Aliitaja kilimo kuwa ni miongoni mwa maeneo ambayo yanaweza kuwekezwa na kupata fedha. Ikiwemo kulima mazao ya biashara, hasa ufuta na mbogamboga. Hata hivyo changamoto ni vijana kutopenda kilimo. Hivyo wabadilike nakufikiri zaidi kujitegemea kuliko kutegemea.
Alitoa wito kwa halmashauri ya manispaa ya Lindi iangalie uwezekano wa kuzikopesha fedha kutoka kwenye mfuko wa vijana ili zianzishe shughuli za kiuchumi. Kwani vijana hao wameamua kujiajiri kupitia michezo. Kwahiyo wana haki ya kukopeshwa kama vikundi vingine vya wajasiriamali wadogo vya vijana, wanawake na walemavu.
Aliahidi kuendelea kuisaidia timu hiyo ambayo inajiandaa kwa mchezo wa ligi ya kombe la shirikisho la Azam( Azam Federation Cup) dhidi ya timu ya Korosho ya wilaya Tunduru, mkoa wa Ruvuma. Mchezo unaotarajiwa kuchezwa mjini Tunduru tarehe 16.12.2020.
Maelezo hayo ya Mbunge yaliungwa mkono na mwenyekiti wa klabu hiyo, Mohammed Bakari (Nguru ) ambaye alisema tofauti za itikadi za siasa, natofauti hizo kuingizwa kwenye michezo zimekuwa na mchango mkubwa wa kudumaza maendeleo ya michezo katika wilaya ya Lindi na mkoa wa Lindi kwa jumla.
Alisema hali hiyo inasababisha wananchi wa Lindi kushindwa kunufaika na fursa zinazotokana na mchezo wa soka. Nikwasababu hakuna timu zinazokwenda katika mji wa Lindi kutoka katika mikoa mingine. Kwani hakuna timu zenye hadhi na uwezo wakuzishawishi timu hizo ziende kucheza Lindi.
" Hivi Simba, Yanga, Azam na timu nyingine kubwa zinawezaje kufikiria kuja Lindi walau kwa michezo ya kirafiki wakati hakuna timu yenye uwezo na hadhi ya kucheza nazo? Matokeo ya yake ni hasara. Timu zingekuja kungekuwa na fursa za kiuchumi na mzunguko wa fedha uneongezeka," alisema Mohamed.
Nae alitoa wito kwa wadau wa michezo na wananchi wa Lindi
wachangie timu hiyo na wasiinasibishe na chama chochote cha siasa. Bali ipo kwaajili ya wana Lindi wote ambao wana itikadi tofauti, lakini itikadi zao wasipeleke kwenye timu hiyo.