Friday, December 4, 2020

Jeshi la polisi kikosi cha Viwanja vya ndege lafanya sherehe za maadhamisho ya siku 16 za kupinga ukatili

 


Jeshi la polisi kikosi cha Viwanja vya ndege "T" kimefanya sherehe za maadhamisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia na watoto kwa kufanya maandamano ya amani yaliyoongozwa na kikosi cha polisi bendi ambayo yalishirikisha majeshi mengine yanayofanya kazi katika viwanja vya ndege ambayo ni Jeshi la wananchi Tanzania kikosi cha 603 KJ, Jeshi la zimamoto na Idara ya Uhamiaji.

Wakati wa ufunguzi wa sherehe hizo za maadhimisho zilizofanyika katika  uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwl.Julius Nyerere Dsm kamishna msaidizi mwandamizi wa polisi Marco Kusekwa alisema "katika vituo vya polisi viwanja vya ndege  tanzania wamekuwa wakikutana na changamoto mbalimbali za kuripotiwa kwa matukio ya unyanyasaji wa kijinsia ambapo katika kipindi cha mwaka jana 2019 jumla ya kesi 13 zilifunguliwa vituoni ikiwemo kesi za ubakaji 1,Rushwa ya ngono 3, Kutelekeza familia 2, kumpa mwanafunzi mimba 2, na kuzuiwa kwa  abiria waliokuwa wakisafiri kwenda nchi za nje kufanya kazi za ndani bila kuwa na vibali kutoka mamlaka husika 5.

Pia Kamanda Kusekwa alisema kuwa idadi hiyo ya kesi imepungua mpaka kufikia kesi 8 kwa mwaka huu wa 2020 kutokana na kuwepo kwa madawati ya kijinsia vituoni, kufikishwa mahakamani kwa watuhumiwa wa kesi hizo   na kuimarishwa kwa mbinu za ukaguzi wa abiria kabla kusafiri kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vinavyofanya kazi Uwanjani hasa Idara ya Uhamiaji.


Aidha aliongeza kwa kusema kuwa kikosi cha polisi viwanja vya ndege kimekuwa kikipokea abiria watanzania wanaorudi/kurudishwa wakiwa tayari wameathirika kisaikolojia kutokana na vitendo vya kikatili walivyofanyiwa katika nchi walizokuwa wakifanya kazi za ndani,hivyo kama kikosi cha polisi huwaunganisha wananchi hao na ndugu zao huku wakati mwingine huwakutanisha na madaktari wataalamu wa magonjwa hayo ya kisaikolojia.


Akizungumza katika maadhimisho hayo kwa niaba ya mgeni rasmi, Elizabeth Thomas (Afisa elimu msingi wilaya ya Ilala) alisisitiza kuwa pamoja na kuwepo kwa vipengele vya kisheria na kiutawala vinavyokataza ukatili huo wa kijinsia bado haitoshi iwapo jamii haitakubali kuwa sehemu ya mabadiliko kama inavyosema kauli mbiu ya mwaka huu " *_Tupinge ukatili wa kijinsia,mabadiliko yanaanza na mimi* ".


Pia aliongeza kwa kusema kuwa ushirikishwaji wa makundi mbalimbali katika jamii ikiwemo viongozi wa dini,viongozi wa kimila n.k utasaidia kwa namna nyingine kutokomeza vitendo hivyo.


Kikosi cha polisi Viwanja vya ndege " T" kinatoa rai kwa wananchi wote hasa wanaotaka kusafiri kwenda nchi za nje kwaajili ya kufanya kazi za ndani wahakikishe kuwa wanafuata utaratibu unaotakiwa pamoja na kuwa na vibali husika ili kukomesha vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia vinavyowapata wanapokuwa huko.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...